Ligi Kuu

‘Mnaomtaka Mpanzu mtamuona Desemba hii’

DAR ES SALAAM: MENEJA wa Habari na Mawasiliano wa Simba Sports Club Ahmed Ally amesema kuwa Wanasimba watamshuhudia mshambuliaji wako mpya Ellie Mpanzu kuanzia Desemba hii.

Akizungumza katika hamasa ya klabu hiyo kuelekea mchezo wao makundi wa kombe la Shirikisho Afrika (CAFCC) dhidi ya CS Sfaxien eneo la Tandika jijini Dar es Salaam Ahmed amesema mshambuliaji huyo mpya wa Simba atasajiliwa rasmi Desemba 15 kwa mashindano ya ndani na kimataifa Januari.

“Desemba 15 litafunguliwa dirisha ndogo la usajili wa ndani na Ellie Mpanzu atasajiliwa hapo kwa maana hiyo mechi yoyote ya ndani baada ya tarehe 15 atakuwa sehemu ya kikosi lakini dirisha la CAF ni mpaka Januari, 2025 kwahiyo mechi yoyote ya kimataifa kuanzia Januari atakuwa sehemu ya kikosi.”

Ahmed pia ametumia fursa hiyo kuiita nguvu ya mashabiki katika mchezo huo akiwataka kujitokeza kwa wingi kujaza uwanja kwani wao ni chachu ya kikosi hicho kufanya vizuri katika uwanja wa nyumbani.

“Hakuna kingine tunachohitaji zaidi ya kujaza uwanja na ushindi ndio maana tukaweka vingilio rafiki. Jukumu la kupata ushindi siku hiyo sio la viongozi peke yao, ni jukumu la kila Mwanasimba. Wewe unayenunua tiketi ya sh 3,000 usione jambo dogo, umeisaidia Simba pakubwa sana.”

Mchezo huo ni wa tatu kwa wekundu wa Msimbazi baada ya kucheza michezo miwili wakishinda mmoja na kupoteza mmoja wakiwa nafasi ya 3 katika kundi A, nyuma ya vinara CS Constantine na FC Bravos walio katika nafasi ya pili.

Simba watashuka dimbani Benjamin Mkapa Jumapili Desemba 15 Dhidi ya CS Sfaxien saa 10 jioni.

Related Articles

Back to top button