Ndoa ya mwana wa tajiri zaidi barani Asia kufungwa ijumaa

MUMBAI: MWANADADA nyota Kim Kardashian na Waziri Mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair ni miongoni mwa wageni wa kimataifa ambao wamewasili Mumbai kwa sherehe ya harusi ya mtoto wa tajiri zaidi barani Asia.
Anant Ambani, mtoto wa Mukesh Ambani, atafunga ndoa na Radhika Merchant, binti wa mfanyabiashara wa maduka ya dawa nchini humo Viren na Shaila Merchant.
Harusi ya siku nne katika jiji la Mumbai kituo cha mwisho katika siku za sherehe za kifahari ambazo familia hiyo imeandaa tangu mwezi Machi, Barabara kuu kuingia eneo hilo zitafungwa hadi sherehe hizo zitakapokamilika siku ya Jumatatu.
Miezi ya sherehe za kifahari ya harusi hiyo ilianza kwa maonyesho ya wasanii wa pop kama Rihanna na Justin Bieber kutumbuiza.
Lakini pia wakazi wa jiji hilo wameanza kupiga kelele wakilalamikia hizo sherehe za matajiri hao kwa sababu hawajui mwisho wa sherehe hizo za tangu mwezi Machi.
Mukesh Ambani mwenye miaka 66, anashika namba 10 kwa matajiri zaidi duniani akiwa na utajiri wa dola za marekani bilioni115, kulingana na Forbes. Kampuni ya Reliance, iliyoanzishwa na babake mwaka wa 1966, ni muungano mkubwa unaofanya kazi katika sekta ya mafuta ya petroli, huduma za kifedha na mawasiliano ya simu.
Anant Ambani ndiye mtoto wa mwisho kati ya watoto wake watatu, ambao wote wako kwenye bodi ya kampuni hiyo. Kijana huyo mwenye umri wa miaka 29 anajihusisha na biashara ya nishati katika kampuni hiyo ya babake na yuko kwenye bodi ya Wakfu wa Reliance.
Siku ya Ijumaa, wanandoa hao watafunga ndoa katika sherehe ya kitamaduni ya Kihindu katika Kituo cha Mikutano cha Jio World Convention.