EPL

Tottenham ni timu ndogo sana- Postecoglou

LONDON:KOCHA wa zamani w Tottenham Hotspur, Ange Postecoglou ameizungumzia Tottenham kwa maneno ya moja kwa moja bila kuficha chochote, akisema wazi kuwa klabu hiyo bado haijafika kiwango cha kuitwa “klabu kubwa”, hasa kwenye suala la matumizi ya fedha.

Kocha huyo aliyeiongoza Spurs kushinda Europa League msimu uliopita kabla ya kutimuliwa, amesema tatizo kubwa la klabu ni kutokubali kulipa mishahara mikubwa kwa wachezaji wa kiwango cha juu. Kwa mtazamo wake, hilo ndilo linawazuia kushindana na timu kama Arsenal, Manchester City au Liverpool.

Ange amesema alipomaliza nafasi ya tano kwenye msimu wake wa kwanza, alihitaji kuimarisha kikosi kwa wachezaji tayari kwa presha ya Premier League. Lakini badala ya kusajili mastaa wakubwa, Spurs waliishia kumchukua Dominic Solanke pamoja na vijana watatu chipukizi.

Alikiri wazi kuwa alikuwa akiwinda majina makubwa kama Pedro Neto, Mbeumo, Semenyo na Marc Guehi, lakini klabu haikuwa tayari kuingia kwenye mbio za mishahara na ada kubwa.

“Niliangalia matumizi yao ya mishahara nikagundua, hawa si klabu kubwa. Klabu kubwa zinatumia pesa kupata wachezaji bora,” alisema.

Mbali na hilo, Ange aligusia pia ile sifa ya “Spursy”, akisema ipo kweli kabisa. Alieleza kuwa kuna hofu ndani ya klabu kuhusu kushinda makombe, hali inayowafanya wakose ujasiri wa kuchukua ‘risk’.

Alisema hata viongozi wa juu wanaonekana kuwa na mawazo ya kushindwa kabla ya mechi kubwa, jambo linaloathiri mentality ya timu.

Kauli hizi zinakuja wakati Tottenham wakiwa kwenye msimu mbaya, wameshuka mpaka nafasi ya 16 kwenye msimamo wa ligi na tayari wamebadilisha makocha mara nyingi ndani ya miaka michache.

Kwa mtazamo wa Ange, mpaka Spurs wakubali kutumia pesa na kubadilisha fikra zao, itakuwa vigumu sana kwao kurudi juu na kupambana kweli kwa makombe makubwa.

Related Articles

Back to top button