Nyumbani

Seleman Mwalimu afarijika kucheza timu Moja na Aziz Ki Wydad AC

MOROCCO:MSHAMBULIAJI wa klabu ya Wydad Athletic Club ya Morocco, Seleman Mwalimu, ambaye ni raia wa Tanzania, ameonyesha furaha yake kufuatia taarifa za kiungo wa Yanga, Stephane Aziz Ki, kujiunga na klabu hiyo kwa msimu ujao.
 
Akizungumza na Azam TV, Mwalimu amesema amefurahishwa sana na uwezekano wa kucheza bega kwa bega na Aziz Ki, ambaye anamwona kuwa na vipaji vya hali ya juu.
 
Amesema taarifa za usajili wa kiungo huyo kutoka Ligi Kuu ya Tanzania zimekuwa zikiripotiwa kwa wingi katika mitandao mbalimbali ya Morocco, jambo linaloonyesha kuwa ligi ya nyumbani inaendelea kupata heshima kimataifa.
 
“Aziz Ki ni mchezaji mzuri sana. Ujio wake kutoka Ligi Kuu ya Tanzania ni jambo linaloonyesha kuwa ligi yetu inaendelea kuwa na ushindani na inatoa wachezaji bora. Ni fursa kubwa kwa wachezaji walioko nyumbani kuona kuwa inawezekana kupata nafasi ya kucheza nje ya nchi,” amesema.
 
Mwalimu ameongeza kuwa uwepo wa Aziz Ki katika kikosi cha Wydad AC utampa nafasi ya kujifunza zaidi kutoka kwa wachezaji wenye viwango vya juu, jambo ambalo litamsaidia kuendelea kukua kiufundi na kiuchezaji.
 
“Wydad AC ni klabu kubwa yenye wachezaji wa kiwango cha juu. Nimefurahi kusikia Aziz Ki anakuja. Naamini kwa pamoja tutasaidiana na kukuza viwango vyetu,” amesema mshambuliaji huyo.
 
Ingawa klabu ya Yanga haijatoa tamko rasmi kuhusu kuondoka kwa Aziz Ki, taarifa mbalimbali zinaeleza kuwa kiungo huyo hatakuwa sehemu ya kikosi hicho msimu ujao, baada ya kusaini mkataba wa miaka miwili na Wydad AC.
 

Related Articles

Back to top button