YANGA VS USM ALGER: Fainali ya jasho na damu kusaka historia

ILIKUWA kama ndoto wakati Yanga wanaianza safari ya michuano ya kimataifa msimu huu, dhamira yao ilikuwa ni kupambana angalau kuingia hatua ya robo fainali.
Yanga walitamani nafasi za juu hasa baada ya kushindwa kufanya vizuri katika michuano
hiyo kwa miaka kadhaa huku watani zao wa jadi, Simba wakiwatania kuwa wao sio timu kubwa kwa sababu hawafanyi vizuri kimataifa.
Watani zao hao walidiriki kuwatania kwa kujivunia na ubora wao wa zaidi ya miaka minne mfululizo wakitinga hatua ya robo fainali Ligi ya Mabingwa Afrika hatua ambayo ilikuwa ni ya mafanikio makubwa kwa soka la Tanzania kwani hakukuwa na timu iliyofikia rekodi hizo.
Mafanikio ya wekundu hao yaliwafanya Yanga kupata wivu na wao kutamani kufanya kitu
ambacho ni zaidi ya walichofanya wenzao.
Yanga wakatangaza kufanya mabadiliko ya uendeshaji kwenda katika mfumo wa kisasa chini ya Ghalib Said Mohamed (GSM) kisha wakafanya uchaguzi na Mhandisi Hersi Said akachaguliwa kuwa Rais sambamba na wajumbe mbalimbali.
Wakati wakiendelea na mabadiliko ya uendeshaji walifanya usajili dirisha kubwa na dirisha
dogo wakionesha dhahiri wamedhamiria kitu msimu huu.
Ubora wa kikosi alichokitengeneza tangu msimu uliopita ulionesha wazi kuwa wanataka mataji ingawa haikufikiriwa awali kama wangefika hatua kubwa ya fainali na hiyo yote ni kutokana na mwenendo wao wa Ligi ya Mabingwa kutokuwa mzuri.
LIGI YA MABINGWA
Wakati wanaanza kucheza Ligi ya Mabingwa katika mchezo wa awali Yanga alicheza na Zalan Rumbek ya Sudan Kusini.
Yanga chini ya Nasreddine Nabi ilitinga hatua ya 32 bora baada ya kuiondosha katika hatua ya kwanza timu hiyo kwa jumla ya mabao 9-0, Mayele akifunga sita kati ya hayo, ‘hat trick’ ugenini na nyumbani.
Mchezo huo wa nyumbani na ugenini ulichezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa,
Dar es Salaam. Kasi waliyoionesha Yanga wengi walizungumza labda ni timu dhaifu wakasubiri kuona mpinzani ajaye ambaye alikutana na Al Hilal ya Sudan.
Hawa walikuwa ni wapinzani wagumu kwa Yanga na waliondosha ndoto yao ya kusonga mbele zaidi kwenye michuano hiyo baada ya kuwafunga jumla ya mabao 2-1.
Mchezo wa kwanza ulichezwa Dar es Salaam, Yanga walilazimishwa sare ya bao 1-1 hivyo katika mchezo wa marudiano uliochezwa Sudan wakafungwa bao 1-0 na kuondosha matumaini yao ya kusonga mbele ila waliangukia katika kapu la Kombe la Shirikisho.
Walipoangukia huko walijipa imani kwamba sasa ni mwendo wa kwenda mpaka fainali
ingawa baadhi ya wadau na wachambuzi wa soka nchini hawakuamini kila mtu akisema
lake ila wao walijifariji hatua moja kwenda nyingine.
SAFARI SHIRIKISHO
Baada ya Yanga kuangukia Kombe la Shirikisho bado watu waliona huenda safari yao
imefika mwisho hasa baada ya kupangwa na mwarabu yaani Club Africain ya Tunisia.
Historia ya Yanga miaka ya nyuma kwa timu za Kiarabu haikuwa nzuri ndio maana
pengine baadhi ya watu waliona anaweza asitoke salama, lakini mambo yalikwenda tofauti kwa matokeo ya kustaajabisha katika hatua hiyo ya mtoano.
Lakini kingine ambacho kiliwafanya watu kuona Yanga anakwenda kutolewa ni historia ya Club Africain katika michuano ya kimataifa ilikuwa bora kwani iliwahi kutwaa taji la Ligi ya Mabingwa Afrika mwaka 1991, ikichukua pia ubingwa wa ligi hiyo mara 13 kuanzia 1947,
1948, 1964, 1967, 1973, 1974, 1979, 1980, 1990, 1992, 1996, 2008, 2015.
Binadamu wanasema soka ni mchezo wa kustaajabisha na wa kikatili na hilo lilifanywa na
Yanga.
Katika mchezo wa kwanza uliochezwa Dar es Salaam walitoka suluhu lakini mchezo
wa pili wa marudiano uliochezwa ugenini Tunisia Yanga iliifunga timu hiyo bao 1-0 matokeo ambayo hayakutarajiwa kwa Watanzania na kutinga hatua ya makundi.
Matokeo hayo sio tu yaliwastaajabisha Watanzania bali wenyeji Club Africain walipata mshtuko. Yalionesha Yanga imejipangaje msimu huu. Mara ya mwisho Yanga ilitinga hatua ya makundi ilikuwa mwaka 2018 kwa hiyo waliweka rekodi nyingine baada ya miaka mitano.
MAKUNDI
Katika hatua ya makundi Yanga iliangukia Kundi D lililokuwa na timu za TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), US Monastir ya Tunisia na Real Bamako ya Mali.
Kwenye hatua hii wapo walioipa Yanga nafasi ya kufuzu hatua ya robo fainali na wengine walibeza wakisema ni ngumu kutokana na aina ya wapinzani lakini wenyewe waliamua kufuta maneno hayo na kuonesha juhudi katika michezo yao.
Yanga iliendelea kushangaza watu kwa kiwango bora katika michezo yake ya nyumbani na ugenini na kwa aina ya uchezaji wao hakika walistahili kufuzu. Takwimu zao za hatua ya
makundi zimeonesha namna gani Yanga ilidhamiria baada ya kumaliza mizunguko sita na kuongoza kundi kwa kufikisha pointi 13.
Waliweka rekodi nyingine kwa kuwa kinara kwenye kundi. Katika michezo sita walishinda minne dhidi ya TP Mazembe nyumbani mabao 3-1 na ugenini bao 1-0 kitu ambacho huko nyuma katika historia ya kukutana nao hawakuwahi kupata matokeo ya namna hiyo.
Walishinda dhidi ya US Monastir nyumbani mabao 2-0, dhidi ya Real Bamako nyumbani mabao 2-0 walitoka sare moja ugenini dhidi ya timu hiyo ya Mali bao 1-1 na kupoteza mchezo mmoja ugenini dhidi ya US Monastir.
Yanga iliongoza kwa kufunga mabao mengi yaani tisa kwenye hatua ya makundi kuonesha namna safu ya ushambuliaji iliyoongozwa na Fiston Mayele na wengine ilivyokuwa bora. Aliyefuatia ni US Monastir alifunga mabao nane.
Lakini pia, katika safu ya ulinzi alifungwa mabao manne sawa na timu hiyo ya Tunisia ikiwa ni machache pia, kuonesha kipa Djigui Diarra na mabeki wake walikuwa makini.
ROBO FAINALI
Yanga iliingia hatua ya robo fainali kwa rekodi za kipekee ikiongoza kundi, ikiwa na mabao mengi ya kufunga na machache ya kufungwa kisha ilipangwa kukutana na Rivers United ya Nigeria.
Baada ya kupangwa na timu hiyo Yanga walifurahi kwa sababu walitaka kulipiza kisasi wakikumbuka kipigo walichopewa na wapinzani hao msimu wa mwaka jana kwa kichapo cha jumla ya mabao 2-0.
Wakati Yanga inafungwa na Rivers hawakuwa vizuri kwa hiyo walifungwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa bao 1-0 kisha walivyokuwa ugenini wakafungwa tena 1-0 tena kwa figisu kitendo ambacho kiliwauma sana.
Ndio maana walivyopangwa nao waliamini kabisa watalipiza kisasi na walifanikiwa baada ya kuwafunga nyumbani kwao mabao 2-0 mchezo wa kwanza uliochezwa Nigeria na kutoka suluhu kwenye Uwanja wa Mkapa.
Kuiondosha timu hiyo iliyokuwa haijapoteza mchezo wowote nyumbani kwao ilikuwa ni fahari kwa Yanga na rekodi ya kipekee na kutinga hatua ya nusu fainali wakiwa wametimiza lengo waliloweka la kisasi.
NUSU FAINALI
Katika hatua hii walikutana na Marumo Gallants ya Afrika Kusini ambayo ilikuwa na rekodi bora pia ya kutopoteza mchezo wowote wa kimataifa nyumbani kwao. Watu waliongea mengi baadhi wakiipa nafasi Yanga na wengine wakisema safari ya Yanga imeishia hapo kwa kuwa waliogopeshwa na kasi ya Marumo ya kimataifa.
Lakini wengine walisema Marumo ni timu iliyokuwa inapumulia mashine kwenye ligi ya Afrika Kusini ikielekea kushuka daraja na kuipa nafasi Yanga na hatimaye walifanya mambo.
Yanga wala haikutishwa kwa sababu hata wao walikuwa na rekodi nzuri nyumbani na ugenini hivyo, walijipanga kwa imani na walisema lazima waende fainali. Katika mchezo wa
kwanza uliochezwa Dar es Salaam, Yanga ilishinda mabao 2-0 na ugenini ikaenda tena kushangaza wengi kwa kushinda mabao 2-1.
Hakika yalikuwa ni matokeo ya kufurahisha kwa mashabiki wake, kwa Watanzania kwa kuwa timu ya kwanza kutinga fainali kwenye michuano hiyo mikubwa baada ya miaka 30.
Simba iliwahi mwaka 1993 mashindano hayo yakijulikana kwa jina la CAF Cup.

FAINALI
Yanga kuingia fainali sio tu ni rekodi yake bali imepeperusha bendera ya Tanzania na Afrika Mashariki kwa sababu ndio timu iliyofanikiwa kufika hatua hizo za juu kwa miaka hii ya karibuni.
Bado kuna waliobeza hawakutaka kuamini kuwa Yanga ni bora bali walisema wamekutana na timu dhaifu ndio maana wamepenya lakini ni maneno tu ya kishabiki.
Sasa Yanga atacheza fainali na USM Alger ya Algeria na mchezo wa kwanza utachezwa kesho (Jumapili) kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa kisha mchezo wa marudiano utachezwa Juni 3, nchini Algeria.
Ni mchezo wa jasho au damu kwa maana Yanga wameonesha wanalitaka kombe na wako tayari kupambana kwa vyovyote vile ili kuwa timu ya kwanza Tanzania kuchukua kombe
hilo la Afrika.
Rais Samia Suluhu Hassan katika kuhakikisha anaiunga mkono timu hiyo alitangaza hivi karibuni kutoa ndege kwa Yanga na mashabiki kwenda Algeria na kupandisha fedha ya
hamasa ya kununua bao kutoka Sh milioni 10 hatua ya nusu fainali hadi Sh milioni 20 kwa kila bao litakalofungwa.
Kwa ubora walionao, Yanga na shauku ni imani kuwa wataendeleza moto wao wa kupambana bila kuwaogopa waarabu bali kuwaheshimu na kujipanga vizuri.
USM Alger mara ya mwisho walivyokutana na Yanga walifungwa hapa mabao 2-1 tena Yanga haikuwa bora sana na kushinda kwao mabao 4-0 mwaka 2018.
Wanakutana na Yanga ikitoka kufanya vizuri kuanzia kwenye ligi wamechukua taji tayari, wamefika fainali ya FA wana wachezaji kama Mayele anayeongoza katika orodha ya wafungaji akiwa amefunga mabao sita akiwa na uchu wa kufumania nyavu.
USM Alger sio timu ya kubezwa ni miongoni mwa timu zinazofanya vizuri ligi ya Algeria na kwa sasa inashika nafasi ya tatu kwa pointi 36 katika michezo 22 ikiwa nyuma mchezo mmoja.
Wanaoongoza ni Constatine yenye pointi 43 na CR Belouizdad yenye pointi 50 katika michezo 23. Katika michuano ya Afrika waliwahi kufika fainali mwaka 2015 na kumaliza nafasi ya pili.
Asilimia kubwa ya wachezaji walionao ni wazawa na wageni wawili kutoka Libya na Botswana. Ni timu inayotoka katika taifa lililoendelea kisoka likishika nafasi ya 34 duniani
katika viwango vya ubora wa soka la kimataifa.
Pamoja na ubora walionao wapinzani bado Yanga ina nafasi ya kumaliza safari yao salama kwa kuweka historia mpya. Maandalizi mazuri, nidhamu ya wachezaji uwanjani na kupigania matokeo yote yanawezekana.
TUJIFUNZE KWA SIMBA
Pamoja na Yanga hadi sasa kuwa na asilimia karibu 60 ya ushindi katika mchezo wa
nyumbani kesho na wengi kuwa na matumaini ya kuendelea kufanya vizuri hata katika mchezo wa marudiano huko Algeria, lakini kazi bado ni kubwa na ngumu.
Tayari baadhi ya watu wanaona kazi kama imeshamalizika, lakini bado na kikubwa Yanga wanatakiwa kujifunza kwa watani zao Simba, ambao mwaka 1993 walipotinga fainali ya Kombe la Caf walijiona kama tayari wametwaa ubingwa.
Katika mchezo wa kwanza, Simba iliwabana Stella Abidjan kwao nchini Ivory Coast na kutoka nayo suluhu na hivyo kila mtu alikuwa na matumaini kuwa katika mchezo wa marudiano kwenye Uwanja wa Taifa (sasa Uhuru) Dar es Salaam, Simba wanakuja kumalizia kazi na kutwaa ubingwa huo.
Kutokana na uhakika huo, iliundwa Kamati ya Ushindi, ambayo pamoja na kupanga mambo mengine ilitangaza barabara ambazo Simba itapita na Kombe hilo la Caf, ambalo wangekabidhiwa na Rais wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi, lakini badala yake walipokea
kichapo cha mabao 2-0 na ndoto zote kuyeyuka.
Yanga wanatakiwa kuelekeza nguvu zao katika maandalizi ya pambano lao la kesho na hilo la Juni 3 badala ya kubweteka na kuanza kufikiria jinsi gani watakavyolibeba taji hilo au jinsi watakavyowakebehi Simba wakiwa timu ya kwanza kuleta taji la Afrika.