Wenger amjia juu Klopp

NEW YORK, Mkuu wa maendeleo ya mpira wa miguu wa FIFA ambaye ni meneja wa zamani wa Arsenal, Arsene Wenger amekosoa maoni ya aliyekuwa meneja wa Liverpool Jurgen Klopp aliyesema Kombe la Dunia la Klabu linaloelekea ukingoni ni wazo baya kuwahi kutokea kwenye soka.
Klopp alinukuliwa katika mahojiano akisema kuwa michuano hiyo iliyopanuliwa ni wazo baya kwa sababu inaongeza idadi ya mechi hivyo kuongeza hatari kwenye afya za wachezaji kimwili na kiakili lakini pia kupunguza uzuri wa mechi kutokana na hali ya hewa ya muda na maeneo mechi zinapochezwa
Akizungumza na waandishi wa habari Wenger ametetea mfumo huo mpya wa kombe la dunia la Klabu akisema kuwa michuano hiyo inapendwa na timu, viongozi na hata mashabiki wa Soka ulimwenguni.
“Kila mtu ana haki ya kutoa maoni na Mimi siungi mkono hata kidogo maoni ya rafiki yangu Jurgen Klopp. Mimi naona kombe Hili la Dunia la Klabu linapendwa na lina mfumo unaohitajika kiushindani”
“Ukiziuliza klabu zote zilizoshiriki kombe hili basi ni hakika asilimia 100 ya Klabu hizo zitataka kucheza tena kombe hili. Hilo ndio jibu bora naloweza kuwapa kwa sasa. Labda tuwaulize mashabiki lakini kwa sababu kuingia kwao kulitabiriwa kuwa kudogo lakini uhalisia ni namba kubwa” – Amesema Wenger
Katika hatua nyingine Wenger amewahakikishia mashabiki wa soka ulimwenguni kuwa Kombe la dunia la 2026 litakuwa na ubora unaostahili kwakuwa watakuwa wamefanyia kazi mapungufu yalioonekana katika Kombe la dunia la Klabu.