Vitinha afanya kweli PSG ikiifumua Spurs

PARIS: MABINGWA watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Paris St Germain (PSG) walionesha roho ya kutokata tamaa baada ya kutoka nyuma mara mbili na kuichapa Tottenham Hotspur mabao 5-3 katika Ligi hiyo, ushindi uliowekwa alama na ubora wa kipekee wa Vitinha ambaye alikiongoza kikosi cha Luis Enrique kuzoa pointi zote tatu.
PSG walionekana kuyumba, wakiruhusu mabao mawili kutokana na makosa ya ulinzi na kuonesha baadhi ya changamoto zilezile zilizopelekea kipigo cha 2-1 dhidi ya Bayern Munich kwenye mechi iliyopita. Hata hivyo, walijibu mapigo kwa utulivu, umakini na ufanisi mkubwa, na kubadili mchezo kwa upande wao katika dimba la Parc des Princes.

Kiungo wa klabu hiyo Vitinha alitupia hat-trick, mabao mawili kwa mipira mizuri ya nje ya boksi na moja kwa mkwaju wa penalti, huku Pacho na Fabian Ruiz pia waingia kambani kwa upande wa PSG.
Baada ya ushindi huo wa nne katika mechi tano, PSG wanaoshika nafasi ya pili kwenye msimamo wa ligi hiyo walihitimisha mchezo wakiwa pungufu baada ya Lucas Hernandez kutolewa kwa kadi nyekundu muda wa nyongeza baada ya kumpiga kiwiko Kiungo wa Spurs Xavi Simons

Katika mchezo wa 500 wa nahodha Marquinhos na klabu hiyo, PSG walionekana kukosa huduma ya beki Achraf Hakimi, huku kiungo Warren Zaire-Emery akicheza kama beki wa kulia.
Ousmane Dembele, ambaye hivi majuzi amerejea kutoka kwenye majeraha, alianzia benchi, huku kijana wa akademi Quentin Ndjantou akiingia kama mshambuliaji chaguo kwanza.




