Unai Simon aendelea kumkosha kocha Spain

BILBAO:GOLIKIPA Unai Simón anaendelea kujiweka juu ya wenzake wote ndani ya timu ya taifa ya Hispania, huku akionekana kuwa chaguo la kwanza la kocha Luis de la Fuente kuelekea Kombe la Dunia 2026, licha ya Uhispania kuwa na kizazi kingine hatari cha magolikipa.

Tangu aitwe kwenye kikosi cha taifa mwaka 2020, Simón amekuwa namba moja karibu kwenye kila mashindano makubwa. Na hata sasa, pamoja na uwepo wa David Raya wa Arsenal, Robert Sánchez wa Chelsea na Joan Garcia wa Barcelona, bado Unai Simón anaendelea kuaminiwa zaidi na benchi la ufundi.

Kocha Luis de la Fuente ameweka wazi msimamo wake, akisema Hispania ina magolikipa kadhaa wanaoweza kuwa namba moja, lakini amefurahishwa sana na kiwango cha Unai. “Ni mchezaji ambaye amekosolewa sana bila haki. Kazi yake imekuwa ya kipekee na ni mchezaji mzuri sana ndani ya kikosi,” amesema.
Kwa mwenendo huu, dalili zote zinaonesha Unai Simón ndiye atakayeilinda Hispania kwenye Kombe la Dunia 2026, tena akiwa mbele ya ushindani mkali.

Swali kwa mashabiki linabaki: nani anastahili kuwa namba moja kuelekea World Cup;Unai Simón, Raya, Sánchez au Joan Garcia?




