Uchaguzi Mkuu Simba Jan 29

KLABU ya soka ya Simba imetangaza kuwa Uchaguzi Mkuu wa timu hiyo utafanyika Januari 29, 2023.
Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi ya Simba Boniface Lyamwike ametangaza tarehe hiyo Dar es Salaam leo wakati wa Mkutano na waandishi wa habari.
“Hii ni dhamana ambayo tumepewa na wanaSimba wanataka viongozi watakaoipa mafanikio timu yao. Kwa hiyo nimewaambia wenzangu tunapaswa kuwa makini ili kuhakikisha jambo hili tunalikamilisha vizuri,” amesema Lyamwike.
Ametoa mwito kwa wagombea watakaojitokeza kuwania nafasi mbalimbali kuzingatia vigezo vinavyotakiwa.
Lyamwike amesema yeye na wajumbe wake wamedhamiria kufanya uchaguzi wa haki na kutompendelea mtu yeyote bila kujali jina wala wadhifa wake.
Mara ya mwisho Simba kufanya uchaguzi mkuu ilikuwa ni Novemba 5, 2018 ambapo Swedi Nkwabi alishinda nafasi hiyo lakini alihudumu kwa mwaka mmoja kabla ya kujiuzulu na nafasi yake kukaimiwa na Mwina Kaduguda ambaye naye aliondoka baada ya klabu kufanya uchaguzi mdogo uliomweka madarakani Murtaza Mangungu.