Twiga Stars kushiriki Pink Ladies Cup

DAR ES SALAAM:TIMU ya Taifa ya Wanawake ya Tanzania, Twiga Stars, inatarajiwa kushiriki mashindano ya kimataifa ya Pink Ladies Cup yatakayofanyika Dubai, Falme za Kiarabu kuanzia Februari 28 hadi Machi 6, 2026.
Mashindano hayo yatazikutanisha timu nne za taifa ambazo ni Tanzania, Russia, Ghana na Hong Kong, huku yakitarajiwa kuwa sehemu ya maandalizi muhimu ya Twiga Stars kuelekea Fainali za Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON 2026) zitakazofanyika nchini Morocco kuanzia Machi 17, 2026.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania TFF, mashindano hayo yataanza Februari 28, ambapo Ghana itacheza dhidi ya Hong Kong kabla ya Tanzania kuvaana na Russia siku hiyo hiyo.
Michuano itaendelea Machi 3, Ghana ikipambana na Russia wakati Hong Kong itamenyana na Tanzania. Siku ya mwisho ya mashindano, Machi 6, Russia itacheza dhidi ya Hong Kong huku Ghana ikimaliza ratiba kwa kukutana na Tanzania.
Ushiriki wa Twiga Stars katika mashindano hayo unatarajiwa kuipa timu hiyo nafasi ya kupima kikosi chake dhidi ya wapinzani wa kimataifa, kuongeza uzoefu kwa wachezaji pamoja na kuimarisha mbinu na mikakati kabla ya kuanza kwa WAFCON 2026.




