Tanzania atwaa ubingwa wa ICC T20 Qualifier B

ACCRA, Ghana
TANZANIA imeandika historia baada ya kutwaa ubingwa wa mashindano ya kufuzu Kombe la Dunia la Kriketi la T20 kwa wanaume, Kanda ya Afrika B (ICC Men’s T20 World Cup Sub Regional Africa Qualifier B), yaliyomalizika nchini Ghana.
Kwa ushindi huo, Tanzania imefanikiwa kufuzu hatua inayofuata ya 2028 T20 World Cup Regional Qualifiers, baada ya kuongoza msimamo wa ligi na kushinda mechi zake zote muhimu katika hatua za awali za mchujo huo wa kuelekea Kombe la Dunia.
Katika mashindano hayo, timu ya taifa ya kriketi ya Tanzania ilionesha kiwango cha juu cha ushindani na uthabiti mkubwa, jambo lililoifanya kung’ara mbele ya mataifa mengine yaliyoshiriki.
Mbali na kutwaa ubingwa, Tanzania pia ilijizolea tuzo binafsi kupitia wachezaji wake waliofanya vizuri ambapo Ajith Augustin alitwaa tuzo ya Best Batsman, Laksh Bakrania akashinda tuzo ya Best Bowler, huku Ivan Selemani akichaguliwa kuwa Player of the Series.
Mafanikio hayo yameendelea kuitangaza vyema Tanzania kimataifa na kuonesha wazi kuwa taifa lina hazina kubwa ya vipaji katika mchezo wa kriketi.
Mashindano hayo yalifanyika kuanzia Machi 22 hadi 30, 2026 jijini Accra, Ghana, yakizikutanisha jumla ya nchi sita ambazo ni Tanzania, Malawi, Saint Helena, Eswatini, Seychelles na wenyeji Ghana.




