Michezo MinginePete

Taifa Queens yaanza vibaya, yalia na waamuzi

TIMU ya taifa ya netiboli, Taifa Queens, imeanza vibaya mashindano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia nchini Afrika Kusini baada ya kufungwa na Namibia mabao 54-40 Agosti 21.

Mashindano hayo ya Afrika yanafanyika Cape Town na washindi wawili wa kwanza wataungana na wenyeji Afrika Kusini na Uganda kuwakilisha Afrika katika Mashindano ya Dunia yatakayofanyika nchini humo kuanzia Julai 28 hadi Agosti 6, 2023.

Mwenyekiti wa Chama cha Netiboli Tanzania (Chaneta), Dk Devotha Marwa amesema kuwa Taifa Queens walipoteza mchezo huo baada ya waamuzi kutowatendea haki.

Amesema kuwa kila wachezaji wa Taifa Queens walipokaribia lango la wapinzani, waamuzi walikuwa wanapiga filimbi wakidai kuwa wachezaji wa Tanzania walicheza faulo.

“Kwa kweli timu yetu ilicheza vizuri, lakini waamuzi hawakuwa ‘fair’ kwetu, kwani kila wachezaji wetu walipofika karibu na lango la wapinzani, walipiga filimbi wakidai kuwa walicheza faulo,” amesema Marwa.

Akizungumzia mashindano kwa ujumla, alisema ni mazuri na yana ushindani mkubwa, kwani kila timu inasaka nafasi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia.

Wakati huohuo, Taifa Queens leo itashuka dimbani kucheza dhidi ya wenyeji Afrika Kusini katika mchezo wa Kundi A, ambalo pia lina timu za Zimbabwe na Botswana.

Kundi B lina timu za Uganda, Malawi, Zambia, Kenya na eSwatini.

Related Articles

Back to top button