Stand United: Bado tuna kazi kubwa mbele

SHINYANGA: KOCHA Mkuu wa Stand United ameweka wazi kuwa licha ya timu yake kupata ushindi muhimu dhidi ya Geita Gold na kusonga mbele katika hatua ya pili ya mtoano, bado kuna kazi kubwa ya kufanya kabla ya kukutana na mpinzani kutoka Ligi Kuu.
Katika mchezo wa marudiano dhidi ya Geita uliochezwa Jana kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani Shinyanga Stand United inayopigania nafasi ya kupanda Ligi Kuu ilishinda mabao 2-0. Mchezo wa kwanza ugenini mkoani Geita walitoka sare ya mabao 2-2.
Akizungumza mara baada ya kumalizika kwa mchezo huo wa marudiano, Kocha huyo amesema kuwa anaipongeza timu kwa kufikia hatua hiyo lakini macho yao sasa yanaelekezwa kwenye mchezo mgumu unaofuata.
“Tunashukuru tumefanikiwa kupata mafanikio. Tumepambana na kuiondoa Geita kwa jumla ya mabao 4-2, lakini bado safari haijaisha. Tunaenda kucheza mtoano na timu kutoka Ligi Kuu, ni mechi nyingine ngumu. Tunahitaji kufanyia kazi mapungufu yetu ili kufanya vizuri na kurejea Ligi Kuu,” amesema.
Stand United iliyoshuka daraja msimu wa 2018/2019 ilionyesha ubora na kujituma katika michezo yote miwili dhidi ya Geita, wakihakikisha wanaendelea na matumaini ya kurejea kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara baada ya kukosekana kwa misimu kadhaa.
Katika hatua inayofuata, Stand United itacheza mechi ya kwanza ya mtoano Julai 3, Shinyanga, kabla ya kusafiri kwa ajili ya marudiano Julai 7,mwaka huu, dhidi ya mshindwa wa mtoano kwa timu zitakazomaliza Ligi Kuu kwenye nafasi ya 13 na 14.
Uongozi wa klabu hiyo umetumia fursa hiyo kuwashukuru mashabiki na wanachama waliounga mkono timu hiyo kwa kujitokeza kwa wingi katika mchezo wa Geita.
“Kwa umoja huu bado tuna nafasi ya kujitokeza kwa wingi kwenye hatua ya pili ya mtoano. Nguvu yako inahitajika sana kuhakikisha tunafikia malengo yetu msimu huu kupanda Ligi Kuu ya Tanzania,” ilieleza taarifa ya klabu hiyo.