EPL

Slot agomea sherehe za tuzo

LIVERPOOL: MENEJA wa Mabingwa wa England Liverpool Arne Slot, amechagua kutohudhuria sherehe za tuzo za Premier League jijini London ambako alitarajiwa pia kupokea tuzo, akisema kujiondoa kwake ni kuonesha mshikamano na wahanga wa tukio la ‘parade’ la ubingwa siku ya Jumatatu.

Slot amechaguliwa kuwa Meneja bora wa msimu wa Ligi kuu na Meneja bora wa mwaka wa Chama cha Mameneja wa Ligi hiyo baada ya kuiongoza Liverpool kutwaa taji lake la 20 la ligi lililoweka rekodi katika msimu wake wa kwanza akiwa na mikoba ya ukufunzi wa klabu hiyo.

Mashabiki wanaokadiriwa kuwa miloni moja walijipanga katika mitaa ya jiji la Liverpool Jumatatu kusherehekea pamoja na wachezaji walipokuwa wakilionesha kombe hilo wakiwa juu ya basi lililo wazi, kabla ya shangwe hiyo kugeuka majonzi baada ya mwanaume mmoja kugonga umati wa watu hao kwa gari.

Watu 65 walijeruhiwa katika tukio hilo na 11 bado wapo hospitalini taarifa zikisema wanaendelea vizuri. Mtuhumiwa katika tukio hilo ni raia wa England mwenye umri wa miaka 53 ambaye bado Polisi hawajaweka hadharani jina na lake yuko mikonononi mwa polisi akikabiliwa na shtaka la kujaribu kuua, lakini pia kwa tuhuma za kuendesha gari bila tahadhari akiwa amevuta dawa za kulevya.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button