Singida baada ya ubingwa Cecafa, macho yote Shirikisho

DAR ES SALAAM:MABINGWA wapya wa michuano ya Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (Cecafa), Singida Black Stars, wamesema ubingwa huo ni chachu ya mafanikio makubwa zaidi wanayoyalenga kwenye mashindano ya kimataifa.
Msemaji wa timu hiyo, Hussein Masanza, alisema kutwaa taji la Cecafa ni mwanzo mzuri na kunawapa nguvu kubwa kuelekea mchezo wao wa kwanza wa Kombe la Shirikisho Afrika (CAF Confederation Cup) dhidi ya Rayon Sports ya Rwanda.
“Tunachukulia hili taji kama motisha muhimu, linaongeza morali ya wachezaji na benchi la ufundi. Tunaamini tukienda Rwanda tutapambana ili kuhakikisha tunapata matokeo mazuri kabla ya kurudiana nyumbani,” alisema Masanza.
Singida Black Stars wanatarajia kusafiri muda wowote kuelekea Kigali kwa mchezo wa kwanza utakaopigwa Septemba 20, mwaka huu, huku lengo lao kubwa likiwa ni kufika hatua ya makundi ya mashindano hayo makubwa barani Afrika.
Katika mchezo wa fainali ya Cecafa uliochezwa jana kwenye Uwanja wa KMC, Singida Black Stars waliibuka na ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Al Hilal ya Sudan, na hivyo kutwaa ubingwa huo kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo.