Africa

Simba, Yanga kivumbi tena kimataifa

SIMBA na Yanga zinarudi kibaruani katika michezo ya Ligi ya Mabingwa na Kombe la Shirikisho Afrika katika michezo itakayochezwa leo na kesho.

Wekundu wa Msimbazi, Simba watakaocheza leo dhidi ya Vipers ya Uganda, wametoka kujeruhiwa mabao 3-0 dhidi ya Raja Casablanca katika mchezo uliochezwa mwishoni mwa wiki iliyopita kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Ni michezo miwili jumla Simba haijapata matokeo baada ya ule wa kwanza kupoteza bao 1-0 dhidi ya AC Horoya ya Guinea uliochezwa ugenini.

Kupoteza huko kwa Simba kunaifanya timu hiyo kushika mkia katika kundi lake la C wakiwa hawajashinda mchezo wowote, huku kinara akiwa ni Raja mwenye pointi sita akitoka kushinda michezo miwili, akifuatiwa na Horoya pointi nne akishinda mchezo mmoja na kupata sare moja na Vipers nafasi ya tatu ikiwa na pointi moja katika mchezo uliochezwa nyumbani kwake Uganda na kutoka sare.

Bado Simba hawapaswi kukata tamaa kwani kuna michezo minne ambayo kama akijirekebisha na kuweka nguvu na kushinda yote anaweza kuingia robo fainali. Na hata akishinda mitatu na sare moja atakuwa na nafasi ya kusonga mbele.

Simba wanahitaji kujipanga na kurejesha ile kasi yao iliyozoeleka miaka iliyopita ambako walikuwa wanashinda ugenini na nyumbani.

SIMBA vs VIPERS
Hii mechi itachezwa Uganda, timu zote hazina matokeo mazuri hivyo pengine kila mmoja anaweza kupambana kuhakikisha anapata matokeo.

Timu zote zinatoka ukanda mmoja ingawa uzoefu wa michuano hii ya kimataifa unatofautiana, Simba akishiriki mara nyingi tofauti na Vipers ambao hawana rekodi nzuri huko.

Vipers imetoka kulazimishwa sare tasa nyumbani kwake dhidi ya Horoya katika mchezo uliochezwa kwenye Uwanja wa St Mary’s Kitende Entebbe, Uganda. Na mchezo wa kwanza walipoteza ugenini Morocco kwa mabao 5-0 dhidi ya Raja Casablanca.

Itataka kupata matokeo mazuri kwenye uwanja wake baada ya kushindwa katika michezo miwili. Wanaweza kuonesha kwamba wao ni bora na hawakubahatisha kutinga hatua hiyo.
Awali, walifahamika kama Bunamwaya kabla ya kubadilisha jina Agosti mwaka 2012 na kuwa Vipers.

Takwimu zao za Ligi Kuu ya Uganda zinaonesha wameshachukua ubingwa wa Ligi Kuu mara tano na makombe mengine ya nchini humo manne. Kikosi cha Vipers kina wachezaji wengi wazawa na wengine wakitoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) wako sita, Burundi mmoja, Sudan Kusini, Angola, Ivory Coast na Nigeria mmoja.

Ni timu nzuri ambayo haipaswi kubezwa kwa sababu licha ya udogo wao kwenye michuano hiyo wameonesha wana kitu na wako imara. Kitendo tu cha kuingia hatua ya makundi kimeonesha wao ni bora msimu huu.

Kwenye Ligi Kuu ya Uganda wanashika nafasi ya tatu baada ya kucheza michezo 15 na kati ya hiyo kushinda minane, sare nne na kupoteza mitatu wakiwa na pointi 28. Mchezo wao wa mwisho wa ligi wametoka kupata sare ya bila kufungana dhidi ya Wakiso Giants.

Wanakutana na Simba ambao wametoka kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Azam FC katika mchezo wa ligi. Timu hii inashika nafasi ya pili kwa pointi 54 katika michezo 23  aliyocheza.
Simba watakuwa na presha ya kutaka matokeo, hasa baada ya kupoteza michezo miwili ya kimataifa kama nilivyoonesha hapo juu.

Wataingia uwanjani kucheza na timu ambayo pengine zinalingana viwango au zimezidiana kidogo, kila mmoja akijua umuhimu wake kwa kumheshimu mwenzake. Utakuwa mchezo mgumu kwa kila mmoja.

Na kama Simba watafungwa na  Vipers, basi hakuna shaka kuwa hatima ya kocha wao Mbrazil, Roberto Oliveira ‘Robertinho’ itakuwa mashakani kwani anaweza kutimuliwa au kuamua kuondoka mwenyewe ili kuepusha shari zaidi.

REAL BAMAKO vs YANGA
Yanga itakuwa ugenini nchini Mali dhidi ya Real Bamako katika mchezo utakaochezwa kesho kwenye Uwanja wa du 26 Mars.

Kipa wa Yanga, Djigui Diarra anarudi nyumbani kwao, hivyo anatarajiwa kuwa ndio mwenyeji wa wenzake nchini humo lakini pia, katika harakati za kwenda kuikabili timu hiyo.

Diarra anawajua vyema Real Bamako kwa kuwa alikuwa anacheza ligi hiyo ya Mali akiitumikia Stade Mallien ya huko. Bamako huu ni msimu wake wa nne kushiriki Shirikisho, mara ya mwisho ilicheza makundi 2014, lakini ikitangulia kutolewa raundi ya awali mwaka 2011 na 2012 iliishia raundi ya pili.

Rekodi yake ipo kwenye Ligi ya Mabingwa ikicheza mara 10, ikimaliza mshindi wa pili
mwaka 1966, miaka sita tangu ilipoasisiwa baada ya kufika fainali na mwaka 1982 ilifika
robo fainali hatua ya juu zaidi tangu fainali ya 1966 na mara ya mwisho kushiriki Kombe la Shirikisho 2018, Kombe la Washindi imecheza mara mbili 1990 na 1997.

Yanga ni timu zoefu katika mashindano hayo baada ya kushiriki kwa miaka tofauti ingawa haikuwa na mafanikio sana.

Imetoka kushinda mchezo mmoja dhidi ya TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) mabao 3-1 katika mchezo uliochezwa kwenye
Uwanja wa Benjamin Mkapa wikiendi iliyopita.

Ni baada ya kutoka kupoteza mchezo wa ugenini dhidi ya US Monastir mabao 2-0. Ushindi uliopita unaifanya Yanga kushika nafasi ya pili kwa pointi tatu nyuma ya Monastir wanaoongoza kwa pointi nne.

Mazembe ya tatu kwa pointi tatu na Bamako wanashika mkia wakiwa na pointi moja baada
ya mchezo uliopita kupata sare ya bao 1-1 dhidi ya Monastir nyumbani. Real Bamako walipoteza mchezo wao wa kwanza dhidi ya TP Mazembe wakiwa ugenini walichapwa mabao 3-1.

Bamako inashika nafasi ya pili kwenye ligi ya Mali baada ya kucheza michezo 10 na kati ya hiyo kushinda sita, sare tatu na kupoteza mmoja ikiwa na pointi 21.

Aidha, wanakutana na vinara Yanga wanaoongoza kwenye ligi ya Tanzania wakiwa wamepoteza mchezo mmoja katika michezo 24 waliyocheza.

Mchezo huo ni muhimu kwa kila timu, Yanga ikisaka ushindi ugenini ili kujiweka katika mazingira mazuri ya kutinga hatua ya robo fainali lakini pia, kwa wenyeji ambao nao wanataka ushindi wakiwa na lengo kama wenzao.

Lolote linawezekana kwa Yanga au Bamako kutegemea na mbinu gani wataingia nazo
katika mchezo huo.

Yanga ikipata sare au ushindi ni matokeo mazuri kwake. Pengine mchezo waliofungwa Tunisia utakuwa umewapa funzo, hivyo wakaingia na mbinu nyingine za kuwawezesha kupata matokeo mazuri.

Kwa mtazamo wangu naamini timu zote mbili zina nafasi ya kutinga robo fainali ikiwa
zitashinda michezo hii na mingine iliyobaki zitajiweka pazuri. Matumaini yapo kwa  mashabiki na Watanzania walioko nyuma yao kuwaombea dua ili wafanye vizuri.

Related Articles

Back to top button