EPL

Sean Dyche afutwa kazi Nottingham Forest

KLABU ya Nottingham Forest imeendelea na utamaduni wake wa kubadilisha makocha mara kwa mara baada ya kumuondoa Sean Dyche, ambaye anakuwa kocha wa tatu kufukuzwa ndani ya msimu huu mmoja.
 
Dyche ameondoka baada ya kudumu kwa siku 114 pekee madarakani, huku taarifa zikithibitisha kuwa uamuzi huo ulifanyika usiku wa manane, saa chache tu baada ya Forest kutoka sare ya 0-0 dhidi ya Wolves. Katika mchezo huo, Forest walipiga mashuti 35 lakini wakashindwa kabisa kufunga bao, jambo lililozidisha hasira kwa uongozi wa klabu.
 
Kabla ya kuondoka, Dyche alikuwa hajashinda mechi tatu mfululizo za ligi, akitoa sare dhidi ya Crystal Palace na Wolves, pamoja na kupoteza 3-1 dhidi ya Leeds, timu pinzani kwenye vita ya kushuka daraja.
 
Forest kwa sasa wako pointi tatu tu juu ya mstari wa kushuka daraja, wakiwa na michezo 12 iliyobaki kumaliza msimu. Inaripotiwa kuwa mmiliki wa klabu, Evangelos Marinakis, hajaridhishwa na timu kushindwa kutumia vipaji vya ushambuliaji vilivyopo kikosini.
 
Kuondoka kwa Dyche kunamaanisha Forest sasa wanatafuta kocha wao wa tatu mbadala ndani ya msimu huu, hali inayoonesha sintofahamu kubwa kwenye benchi la ufundi la klabu hiyo.

Related Articles

Back to top button