EPL

Salah atajwa PFA

LONDON: Mshambuliaji wa Mabingwa wa Ligi Kuu ya England Liverpool, Mohamed Salah ni miongoni mwa wachezaji sita walioteuliwa kuwania tuzo ya Mwanasoka Bora wa Mwaka wa Chama cha Wanasoka la Kulipwa PFA.

Nyota huyo wa Misri mwenye umri wa miaka 33 alichangia pakubwa katika ushindi wa taji la Ligi Kuu la Liverpool msimu uliopita kwa mabao 29 na asisti 18. Awali alichaguliwa kuwa Mwanasoka Bora wa Mwaka na Chama cha Waandishi wa Habari za soka akipata karibu asilimia 90 ya kura, na sasa ndiye anayepewa nafasi kubwa ya kutwaa tuzo hiyo ya PFA.

Salah amejumuishwa kwenye orodha hiyo na mchezaji mwenzake wa Liverpool Alexis Mac Allister, Declan Rice wa Arsenal, Cole Palmer wa Chelsea, mshambuliaji wa Newcastle Alexander Isak, na kiungo wa Manchester United Bruno Fernandes.

Kuonekana kwa jina la Cole Palmer, ambaye alishinda tuzo ya Mchezaji Bora Chipukizi wa Mwaka wa PFA kwa msimu wa 2023/24 kwenye orodha hiyo kumepokelewa kwa mshangao kutokana na kutofanya vizuri na Chelsea msimu uliopita.

Declan Rice alicheza kwa mafanikio katika safu ya kiungo ya Arsenal, akifunga mabao tisa idadi kubwa zaidi katika maisha yake ya soka akiongeza asisti 10 katika mechi 52 za michuano yote.

Mshambuliaji wa Sweden Alexander Isak aliifungia Newcastle mabao 23 akiisaidia kufuzu Ligi ya Mabingwa msimu ujao na kumaliza ukame wa miaka 56 wa kutwaa mataji kwa kushinda Kombe la Ligi.

Bruno Fernandes yeye alikuwa mmoja wapo wa wachezaji wachache wa United waliong’aa katika msimu mbaya zaidi wa United ndani ya ligi kuu tangu 1973/74, akiwa na mabao manane ya ligi na asisti 10. Sherehe za tuzo za mwaka huu zitafanyika huko Manchester Agosti 19.

Related Articles

Back to top button