Rose Muhando achumbiwa nchini Kenya

NAIROBI: MSANII maarufu wa nyimbo za Injili kutoka Tanzania, Rose Muhando, anayejulikana kama Malkia wa Gospel, ametangaza rasmi kuolewa na Bishop Robert Bob Lumbasi, raia wa Kenya ambaye ni Bishop, Msanii wa Injili na askari wa cheo cha juu nchini humo.
Bishop Lumbasi alitangaza habari hizo baada ya kumvisha pete ya uchumba Rose Muhando katika tukio lililofanyika nchini Kenya, hatua iliyoashiria mwanzo wa safari ya ndoa kwa wawili hao.
Akizungumza baada ya tukio hilo, Lumbasi amesema kuwa mahari tayari imelipwa, na kwa sasa Rose Muhando “hayuko sokoni tena”.
“Mahari nimeshalipa, sasa kinachosubiriwa ni harusi,” amesema Bishop Lumbasi mbele ya waumini na waandishi wa habari.

Harusi ya Rose Muhando na Bishop Robert Lumbasi imetangazwa rasmi, huku mashabiki wa Injili kutoka Tanzania na Kenya wakisubiri kwa hamu kutangazwa kwa tarehe rasmi ya ndoa.
Wachambuzi wa masuala ya muziki wa Injili wanasema harusi hiyo huenda ikawa moja ya harusi kubwa zaidi kuwahi kushuhudiwa nchini Kenya, ikizingatiwa umaarufu na heshima waliyonayo wawili hao katika huduma ya Injili.
Baada ya tangazo hilo, kanisa lililipuka kwa shangwe, waumini wakisikika wakisema “Harusi tunayo!” huku wakishangilia kwa furaha kubwa mara baada ya Bishop Lumbasi kuthibitisha kuwa Rose Muhando tayari amechumbiwa.

Ikumbukwe kuwa hivi karibuni, Rose Muhando aliwahi kuweka wazi kuwa aliwahi kuishi na wanaume, lakini hakuwahi kufunga ndoa rasmi kauli iliyowagusa wengi na kuzua mjadala mkubwa.
Tangazo la sasa limepokelewa kama ukurasa mpya wa maisha yake binafsi na ya kiroho.
Mashabiki wa Injili sasa wanasubiri kwa hamu kuona tarehe ya harusi ikitangazwa rasmi, huku wakimtakia heri Malkia wa Gosper katika safari yake mpya ya maisha ya ndoa.




