Rose Mhando akataa Kuchonganishwa na Msama

DAR ES SALAAM: MWIMBAJI nguli wa muziki wa Injili, Rose Mhando, amesema kuwa Mkurugenzi wa Msama Promotions, Alex Msama, ni zaidi ya baba kwake.
Ameeleza kuwa tangu aanze safari yake ya uimbaji wa nyimbo za Injili, amekuwa akifanya kazi na Msama kwa ushirikiano wa karibu, bila dhuluma yoyote.
Rose amesema kuwa yeye pamoja na baadhi ya wasani wenzake wa muziki wa Injili hawawezi kutaja mafanikio yao bila kumtaja Msama, ambaye hivi karibuni alitunukiwa tuzo ya Muandaaji Bora wa Muziki wa Injili wa Wakati Wote.
Kauli hii ya Rose imekuja baada ya kuwepo kwa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zinazodai kuwa aliwahi kudhulumiwa haki zake na Msama. Akizungumzia madai hayo, Rose amesema ameshtushwa na kusikitishwa na taarifa hizo, akisisitiza kuwa hazina ukweli wowote.