Mastaa

Rihanna aweka ubilionea pembeni, aingia dukani kama mama wa kawaida

MAREKANI: Licha ya kuwa bilionea na mmoja wa mastaa wakubwa wa muziki duniani, Rihanna ameonesha kuwa linapokuja suala la familia, yeye ni mama wa kawaida tu kama wanawake wengine.

Muimbaji huyo maarufu alionekana Jumatatu, Februari 9, 2026, akifanya manunuzi ya mboga mboga na mahitaji ya jikoni yeye mwenyewe katika supermarket ya Bristol Farms, West Hollywood, Los Angeles.

Tofauti na wengi wanavyoweza kutegemea kwa mtu wa hadhi yake, Rihanna hakuwa na misafara wala wasaidizi wa kumfanyia kila kitu. Aliingia dukani kama mteja wa kawaida, akichagua bidhaa na kusukuma toroli lake mwenyewe.

Video na picha zilizosambaa mitandaoni zikimuonesha ndani ya duka hilo zimewavutia wengi, huku mashabiki wakisifia unyenyekevu wake. Wengi walisema angeweza kuwatuma wasaidizi wake kufanya manunuzi, lakini alichagua kufanya mwenyewe kama mama anayejali familia yake.

Rihanna, ambaye sasa anatambulika pia kama mfanyabiashara mkubwa na bilionea kupitia miradi yake ya urembo na mitindo, ana watoto watatu na rapper A$AP Rocky. Wana wawili wa kiume, RZA na Riot, pamoja na mtoto wa kike Rocki Irish.

Pamoja na utajiri na umaarufu wake, tukio hilo limeonesha upande mwingine wa maisha yake, kwamba nyuma ya jina kubwa la staa, bado kuna mama anayehangaika jikoni na familia kama ilivyo kwa wanawake wengi duniani.

Kwa kifupi, fedha na mafanikio vinaweza kubadilisha maisha, lakini haviwezi kubadilisha moyo wa mama.

Related Articles

Back to top button