EPL

Ratcliffe: Kutokuwa maarufu Man United kunaanza kuzaa matunda

MANCHESTER: Mwenyekiti wa kampuni ya INEOS na mmiliki mwenza wa timu ya Manchester United, Jim Ratcliffe, amesema maamuzi magumu aliyoyachukua ambayo yalimfanya asiwe maarufu miongoni mwa mashabiki sasa yanaanza kuonesha matokeo chanya ndani ya klabu hiyo.

Ratcliffe, ambaye alinunua hisa katika klabu hiyo ya Ligi Kuu England miaka miwili iliyopita, amefanya mabadiliko kadhaa yenye utata katika uongozi na uendeshaji wa klabu hiyo ya Old Trafford.

Hatua hizo zimehusisha kupunguza wafanyakazi pamoja na kuwaondoa makocha waliokuwa wakikosolewa kwa kushindwa kufikia matarajio, akiwemo Erik ten Hag na Ruben Amorim.

Katika kipindi hicho, Ratcliffe na wamiliki wenzake wa familia ya Glazer wamekuwa wakikumbwa na maandamano kutoka kwa mashabiki waliokasirishwa na mwenendo wa timu.

Hata hivyo, hali imeanza kubadilika baada ya kocha wa muda, Michael Carrick, kuiongoza timu katika mwamko mpya wa matokeo mazuri. United imepata ushindi mara nne na sare moja katika michezo ya hivi karibuni, hatua iliyoiweka tena katika mbio za kuwania kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu ujao.

Akizungumza na Sky News Jumatano, Ratcliffe alilinganisha maamuzi yake na yale ya wanasiasa wanaolazimika kuchukua hatua zisizopendwa ili kurekebisha mambo makubwa.

“Nimeona hali kama hii katika klabu ya mpira. Ukifanya mambo magumu ambayo tulihisi ni lazima yafanyike Manchester United, unaamini ni sahihi, lakini kwa muda fulani unakuwa haupendwi,” alisema.

Aliendelea kusema: “Nimekuwa sipendwi sana Manchester United kwa sababu tumefanya mabadiliko mengi. Lakini kwa mtazamo wangu, ni kwa ajili ya mema. Na sasa tunaanza kuona dalili ndani ya klabu kwamba hatua hizo zinaanza kuzaa matunda.”

Ratcliffe, mwanzilishi wa kampuni ya kemikali ya INEOS, anaamini kuwa licha ya upinzani wa awali, mwelekeo mpya wa uongozi na maamuzi ya kiutendaji yanaanza kuirejesha Manchester United katika ushindani wa juu.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button