Kwingineko
PSG yatawala usiku wa tuzo za Globe Soccer

DUBAI:USIKU wa jana Jumapili, Desemba 28, 2025, macho ya dunia ya soka yalikuwa Dubai ambako tuzo za Globe Soccer zilitolewa, na Paris Saint-Germain (PSG) ikaondoka kifua mbele baada ya kufanya vizuri kupita kiasi.
PSG, ambayo ilimaliza mwaka 2025 kwa kutwaa mataji sita ikiwemo Ligi ya Mabingwa Ulaya, ilikusanya jumla ya tuzo saba na kuthibitisha ubora wake ndani na nje ya uwanja. Klabu hiyo ilitangazwa kuwa Klabu Bora ya Wanaume, ikiwaacha nyuma vigogo wengine wa Ulaya.
Nyota wao Ousmane Dembélé aliibuka kuwa Mchezaji Bora wa Dunia, huku kipaji chipukizi Désiré Doué kikitwaa tuzo ya Mchezaji Kijana Bora wa Mwaka. Kwa upande wa uongozi, rais wa PSG Nasser Al-Khelaïfi alichaguliwa kuwa Rais Bora wa Mwaka.
Benchi la ufundi halikubaki nyuma, ambapo Luis Enrique alitangazwa Kocha Bora, na Luis Campos akachukua tuzo ya Mkurugenzi Bora wa Michezo. Kiungo Vitinha naye aliongeza heshima kwa PSG baada ya kutangazwa Kiungo Bora wa Mwaka 2025.
Mafanikio hayo yote yalitokana na msimu wao wa kihistoria wa 2024/25, uliowaweka PSG kileleni Ulaya na duniani.
Wakati Ousmane Dembélé akitwaa tuzo ya Mchezaji Bora Duniani, Vitinha akachaguliwa Kiungo Bora, Lamine Yamal akatangazwa kuwa Mshambuliaji Bora, huku Désiré Doué akipewa tuzo ya Mchezaji Chipukizi Bora wa Mwaka; Luis Enrique aliibuka Kocha Bora, Cristiano Ronaldo akachukua tuzo ya Mchezaji Bora wa Mashariki ya Kati, na Paris Saint-Germain (PSG) ikahitimisha kwa kutangazwa Klabu Bora ya Wanaume.




