Muziki

Omari K atangaza ujio wa albamu yake

MSANII wa kizazi kipya anayefanya vyema nchini Marekani, Omari K, ameweka wazi ujio wa albamu yake fupi (EP) aliyoipa jina la ‘I am Bantu Music’, itakayotoka hivi karibu kwenye majukwaa (platforms) yote ya kupakua na kununua muziki duniani.

Omari K ni miongoni mwa wasanii wachache sana wa kitanzania wanaoishi Marekani wenye mafanikio makubwa kwenye tasnia ya muziki kama kushinda tuzo nne pamoja na kufanya kazi na mastaa wakubwa hapa Bongo kama Alikiba, Chino Wanaman na kolabo na Malkia wa mipasho, Khadija Omari Kopa.

Rapa huyo ambaye ni mmiliki wa lebo ya Upendo Records na chombo cha habari, Upendo Records Media, ameweza kujizolea maelfu ya mashabiki ndani na nje ya Marekani akitumia lugha tofauti tofauti kama Kizigua,Kiswahili, Mai Mai na Kingereza.

Omari K ameiambia Spotileo kuwa ndani ya EP hiyo mpya kutakuwa na nyimbo kali tano zitakazoendelea kumpa heshima yeye na tasnia ya muziki ya Tanzania hivyo mashabiki wakae mkao wa kuburudika.

“I am Bantu Music ni EP iliyoshiba, inayoendelea kunipa heshima, nimeshafanya mambo makubwa kwenye huu muziki na mwaka huu nitaendelea kuipeperusha bendera ya Tanzania hapa Marekani kwenye tasnia ya muziki na hata filamu.

“Pia tayari nimetoa kionjo (trailer) ya filamu yangu mpya inayoitwa Queen of The Ring itakayoanza kuoneshwa kwenye majumba ya sinema hapa Marekani Oktoba mwaka huu hivyo naomba sapoti kwa mashabiki zangu wa Tanzania, Kenya na Afrika Mashariki yote kwani nawawakilisha vizuri hapa Marekani,” amesema Omari K ambaye mashabiki wamempachika jina jipya la K Boss.

Related Articles

Back to top button