
DAR ES SALAAM:MSANII wa vichekesho nchini, Neila Manga, ametangaza kuanzisha kampeni maalum ya kuwatetea wanaume ili wapate uhuru wao katika jamii.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Neila Manga alichapisha video akieleza rasmi kuanzishwa kwa kampeni hiyo aliyoiita “Freedom for Men”, yenye lengo la kusimamia haki na nafasi ya mwanaume katika familia na jamii kwa ujumla.
Katika ujumbe wake, Neila amesema kuwa mwanaume ni kichwa cha familia na anapaswa kupewa nafasi ya kuongoza bila kubanwa au kupangiwa maisha yake.
“Nimeanzisha kampeni yangu ya kuwatetea wanaume inayoitwa Freedom for Men. Wanaume na uhuru wao waacheni wawe huru,” amesema Neila Manga.
Ameongeza kuwa lengo kuu la kampeni hiyo ni kuhamasisha heshima kwa nafasi ya mwanaume, hasa katika mahusiano na familia.
“Mwanaume ndiye kichwa cha familia, ndiye mwanga na anayepaswa kukuongoza. Wewe mwanamke unayempangia mwanaume wako nini cha kufanya, awe wapi au awe na nani, hata kama una hela au huna hela, acha tabia hiyo. Waacheni wanaume wawe huru,” amesisitiza.
Kauli hiyo imezua mjadala mpana mitandaoni, ambapo baadhi ya watu wameunga mkono wazo hilo huku wengine wakilipinga, wakidai linahitaji mjadala mpana zaidi kuhusu usawa na majukumu ya kijinsia.




