Nandy akiri kumlipisha yammy baada ya kuondoka

DAR ES SALAAM:MSANII wa muziki wa Bongo Fleva, Faustina Charles maarufu kama Nandy, amethibitisha kuwa kweli alimlipisha kiasi fulani cha fedha aliyekuwa msanii wake Yammy baada ya kuondoka kwenye lebo ya African Princess.
Hata hivyo, Nandy amesema kiasi hicho kilikuwa kidogo kwa kuwa alizingatia hali ya msanii huyo kijana bado kujitafuta kwenye muziki.
“Ni kweli nilimlipisha, lakini nilimpunguzia kwa sababu bado ni msanii anayeanza, bado anajitafuta,” amesema Nandy.
Kauli hiyo imekuja kufuatia madai kutoka kwa Yammy, msanii wa kwanza kusainiwa kwenye lebo ya African Princess, ambaye hivi karibuni alidai kuwa alimwalika Nandy kwenye uzinduzi wa wimbo wake mpya lakini hakufika.
Akijibu madai hayo, Nandy amekanusha kutopokea mwaliko huo na kueleza kwa kina kilichotokea.
“Yammy alisema alimpigia simu kunialika lakini kiukweli sijaona simu yake. Nilimtafuta kwenye DM (Instagram), nikamuuliza: umenipigia siku zipi mbona sijaona simu?” alisema Nandy.
Nandy aliongeza kuwa kama kweli alitaka kumpata, Yammy alikuwa na njia nyingi za kufanya hivyo.
“Anayo namba ya mdogo wangu, dada yangu, hadi ya mtoto wangu Naya — angeweza kunipata. Ila yeye akasema alibiwa simu na hakuwa na namba. Na hata nilivyompigia hakuniambia ana uzinduzi, huenda wakati huo hakuwa amepanga bado,” alifafanua Nandy.
Kwa sasa, mashabiki wanasubiri kuona kama wawili hao wataweza kurekebisha tofauti zao na kuendeleza mahusiano yao ya kikazi kama ilivyokuwa zamani.
Japo Nandy amesema kuwa hakuna shida yoyote inayoendelea baina yao lakini kwa hali hiyo kunakitu unaona hakipo sawa.




