Nana Dollz aweka wazi anavyotoka na mbunge wa Kenya

DAR ES SALAAM: MUIGIZAJI na mwanamitindo kutoka Tanzania Nasma Hassan, maarufu Nana Dollz, ameweka wazi namna anavyotoka na Mbunge wa Kasarani na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa SportPesa, Ronald Karauri.
Nana ameweka hayo wazi katika mahojiano na Wasafi TV alipokuwa akifafanua uvumi, mizozo na gumzo lililovuma mtandaoni kwa miezi kadhaa huku akieleza msimamo wake na namna walivyokutana na mbunge huyo na kuanza uhusiano wao wa kimapenzi.
Mahojiano hayo ya Wasafi TV yalitokana na madai ya kulipuka kutoka kwa mwanablogu Mtanzania Mange Kimambi, ambaye mapema Aprili 2025 alivujisha picha na video zinazodaiwa kumuonesha Nana akiwa nyumbani kwa Karauri Nairobi. Picha hizo, ambazo ni pamoja na Nana akiwa katika sebule ya mbunge huyo na kwenye matembezi ya kimahaba, zilichochea uvumi wa mahusiano ya kimapenzi kwa wawili hao.
Kimambi alimshutumu Nana kwa kuwafuata wanaume matajiri ili kujinufaisha kifedha, hata akidai alimshinikiza Karauri kufadhili jumba la kifahari na bwawa la kuogelea huku akidai mbunge huyo Karauri alitengana na mkewe, Kapteni Ruth Karauri, karibu miaka mitatu iliyopita, jambo lililoongeza utata wa sakata hilo.
Katika mahojiano, Nana amesema “Nilikutana naye alipokuwa akiishi peke yake,” huku, akisisitiza kwamba uhusiano wao ulianza baada ya ndoa ya Karauri kuisha. “Hakuwa na mke wake tulipoanza. Watu hawajui habari kamili, lakini ni wepesi wa kuhukumu. “Sijawahi Kukutana na Mwanaume Kama Yeye” alisifia.
Nana alipuuzia mbali dhana ya kuwa amevunja nyumba ya mbunge huyo, akidai kwamba uhusiano wao ulijengwa juu ya kuheshimiana na kuelewana, na si vinginevyo.
“Sijawahi kukutana na mwanaume mwerevu na mkali kama mpenzi wangu,” amesema, sauti yake ikionesha kuvutiwa na mbunge huyo.
“Mimi sio mtu wa kijamii tu,” alisisitiza. “Mimi ni mwerevu, mwenye elimu, mchapakazi, mwenye fadhili, na mcha Mungu.” Alieleza muigizaji huyo aliyefahamika kama Regina Lewa kwenye tamthilia ya Pazia huku akigusia miradi yake ya ujasiriamali, pamoja na jumba la kisasa ambalo anaripotiwa kujenga.
Ingawa alikubali msaada wa kifedha wa Karauri, kama vile michango ya kila mwezi, alisisitiza uhuru wake mwenyewe. “Naelekeza mapato yangu kwenye miradi yangu. Sijakaa kusubiri mtu yeyote anikabidhi vitu.”
“Nina haki ya kumpenda yeyote ninayemtaka,” Nana alitangaza, akirejea maoni aliyoshiriki kwenye Instagram. “Uhusiano wangu sio lazima uwe wa maana kwa mtu yeyote isipokuwa sisi. Sisi ni watu wazima, na tunajua tunachofanya. Hakuna mtu anayeweza kuniaibisha kwa chaguo langu.”
Mahojiano ya awali, aliyofanya Septemba 2021 na Wasafi TV, alifafanua kuwa mpenzi wake wa zamani baba wa binti yake Soraya amemsaidia katika kulipa kodi na mafuta, lakini amekuwa msumbufu.