Mr. Chuzi aliyempika mkude simba akapikika

DAR ES SALAAM: KATIKA upepo wa simulizi za Instagram, nyota mwenye sura nyingi katika sanaa muigizaji, mchekeshaji, mwandishi wa tamthilia na mbadili-sauti mahiri, Mussa Kitale ‘Mkude Simba’, maarufu kama Bwakila, amefungua ukurasa wa kumbukizi za safari yake ya ubunifu.
Safari ambayo chanzo chake hakikuwa studio, bali mikono ya mtu mmoja muhimu sana katika tasnia ya filamu na tamthilia nchini: Jumanne Kigangala, ‘Mister Chuzi’, yule ambaye wengi humzoea kama Tuesday Kihangala.
Kwa miaka mingi, jina la Mr. Chuzi limekuwa kama mhimili wa hadithi nyingi zilizojenga sura ya tasnia yetu. Ameongoza na kusimamia kazi kubwa zilizoacha alama zisizofutika zikiwemo Tamthilia kama, Rangi ya Chungwa (2002/2003), Valentine Day (2000/2001), Ua Jekundu (2004/2005), Jumba la Dhahabu (2006/2007), Jasmine (2010), Closed Chapter (2017) na Picha Yangu (2024).
Kwa upande wa filamu, ametikisa na Kaburi la Sophia, Harusi ya Candy na Safari.

Ametokea Kinole, Morogoro, lakini athari yake imeenea taifa zima. Kama mwalimu asiyekuwa na darasa rasmi, Mr. Chuzi amejenga misingi ya wasanii wengi ambao leo wanaishi kupitia kazi zao, na Kitale anasema yeye ni mmoja wa waliofunguliwa milango ya safari yao ya sanaa na mtu huyu.
Kitale anakumbuka mwaka 2007, kipindi ambacho tasnia ilianza kumgeukia kwa jicho la pekee. Ingawa tayari alikuwa ameonekana kwenye tamthilia kadhaa, ilikuwa “Jumba la Dhahabu” iliyofanya sauti yake isikike mbali zaidi. Hapo ndipo Mr. Chuzi alipochoma mwanga wake wa ushauri:
“Sitaki uigize kama kawaida. Nataka uwe teja mtumiaji wa dawa za kulevya. Nenda ukalete uhalisia,” anasimulia Kitale.
Kwa mtu mwingine, huenda ingekuwa kikwazo. Kwa Kitale, ilikuwa changamoto ya kuzaliwa upya kisanaa. Akaingia mitaani, si kwa kujificha, bali kujifunza. Miongoni mwa waliompa sura ya uhusika alikuwa Dame wa Mwananyamala—miondoko, mitetemo, na mwendo wa kubeba mateja wa “original”. Kitambaa kichwani akakichukua kwa Akindu wa Manzese, koti akavutiwa na mhusika mbaya wa filamu za Suniel Shetty, na plasta shavuni akaiiga kwa Nell, msanii wa enzi zile.

Vitu vidogo vikawa mbegu. Mbegu zikamea ikawa Kitale wa kipekee, uhusika ambao haukuwa kichekesho tu ulikuwa masimulizi ya maisha halisi ya watu waliopo pembeni ya jamii.
Baada ya kumwangalia akichanua uhalisia huo, Mr. Chuzi alimwambia: “Hii staili itakufikisha mbali. Wengine wataiga, lakini hawataweza kubeba ule undani ambao ni wako.”
Na kweli, ikawa hivyo. Uhusika wa Kitale ukawa dira, ukawa chapa yakeukawa historia.
Mbali na Mkude Simba na taswira ya Bwakila wa EFM, hiki ndicho kiini cha safari yake: msanii aliyegunduliwa, akalelewa, akahimizwa, na hatimaye akasimama kwa miguu yake kupitia macho ya mtu mmoja—Mr. Chuzi, aliyemtia mwanga mahali ambapo wengine wasingeuona.
Na mwisho wa simulizi yake, Kitale anaweka nukta ya shukrani: “Shukrani za dhati kwa Mr. Chuzi – mtu aliyeniweka kwenye njia sahihi ya sanaa.”




