Mpira wa mikono waomba sapoti

DAR ES SALAAM: CHAMA cha Mpira wa Mikono Tanzania kimeomba wadau na makampuni mbalimbali kuwasapoti wajiandae vizuri na mashindano ya kanda ya tano Afrika yatakayofanyika Uganda kuanzia Mei 6, mwaka huu.
Kwa mujibu wa Makamu wa Rais wa chama hicho Anna Kasiga, timu imeanza maandalizi ya kujiweka imara na tayari lakini ili kufanikisha mpango wao wa safari na kuwakilisha wanahitaji sapoti ya wadau.
“Naomba makampuni, mashirika yatusaidie kwa chochote ili tuweke kambi katika mazingira mazuri, tutakuwa hapa Dar es Salaam na baadaye tutahamishia kambi yetu mkoani Tanga kwa maandalizi ya mwisho,”amesema.
Kasiga amesema timu yao ni nzuri sana kwani ilishika nafasi ya tatu kwenye mashindano ya Afrika yaliyofanyika nchini Ivory Coast mwaka jana.
“Mwaka jana tulikuwa mabingwa wa tatu wa Afrika mashindano yaliyofanyika nchini Ivory Coast kati ya timu nane. Wengi hawaujui hawatujui kwasababu hawatuoni kwenye vyombo vya habari,”amesema.
Amesema imani yao kubwa katika michuano hiyo ijayo ni kuendeleza ushindi. Nchi nyingine zitakazoshiriki ni Kenya, Uganda, Djobouti na Sudan Kusini.