Miss Tanzania wamlilia Hasheem Lundenga

DAR ES SALAAM: MRATIBU wa shindano la urembo la Miss Tanzania, Hashim Lundenga amefariki dunia leo Jumamosi April 19, 2025 huku waandaaji wa shindano hilo wakisema wamepokea kwa masikitiko makubwa.
Lundenga amefariki dunia katika Hospitali ya Kitengule iliyopo Tegeta jijini Dar es Salaam. Taarifa ya kifo chake imethibitishwa na Msemaji wa shindano hilo Hiddan Rico.
Rico amesema watamkumbuka Lundenga kama mtu mwenye mchango katika sekta hiyo ya urembo.
“Ni kweli amefariki na taratibu za mazishi zinaendelea, lakini kwa taarifa nilizopokea huenda akazikwa kesho,”amesema na kuongeza kuwa msiba upo nyumbani kwake Bunju.
Taarifa zilizopo ni kuwa Lundenga aliumwa kwa muda mrefu alipata kiharusi ‘stroke’ na alilazwa kwenye Hospitali Muhimbili baadaye Mlongazila na alikuwa akiendelea na matibabu.
Alisema hali yake ilibadilika jana akapelekwa kwenye Hospitali ya Itengule ambapo alifariki.
Lundenga ndiye aliyefanya mashindano ya urembo Tanzania kupata umaarufu mkubwa miaka miaka ya 1994-2018. Aliwahi pia,kufanya kazi kwenye kamati za klabu ya Yanga.