Kwingineko

Messi alitaka kunisaidia niwe mchezaji bora duniani- Neymar

'Hakutaka kabisa niondoke Barcelona'

NEYMAR alipoulizwa na Romario kuhusu maisha yake Barcelona hadi sakata lake la kutimka na kwenda PSG alijibu: “Nilitumia miezi 6 ya kwanza pale Barça nikiwa na wasiwasi mwingi. Nilijisikia nisiye wa maana, niliona siwezi kumpiga chenga mtu yeyote, siwezi kumzidi mtu yeyote, kila kitu nafanya vibaya kabisa!’
“Kulikuwa na siku moja nilivunjika moyo sana. Ilikuwa mapumziko ya kipindi cha kwanza. Nakumbuka siku hiyo hadi leo, ilikuwa dhidi ya Athletic Bilbao. Niliingia kwenye chumba cha kubadilishia nguo nikiwa nimejikasirikia sana. Nilikuwa nacheza vibaya mno. Niliingia chooni na kuanza kulia peke yangu, nikijiuliza ‘ninafanya nini?’ Kisha Messi akagonga mlango. Aliniuliza: ‘Kwa nini unalia?’ Nikasema, ‘Hapana, niko sawa, niko sawa.’
 
“Dani Alves naye akaingia, na Messi akasema: ‘Tuliza moyo, tupo hapa kukusaidia. Tunataka ucheze soka lako bora kama ulivyofanya kule Santos, bila presha yoyote. Ukihitaji chochote, unaweza kutegemea msaada wangu.’
“Baada ya hapo nilianza kuwa na kujiamini zaidi. Nilikuwa na hamasa kubwa ya kucheza, na kila kitu kilianza kwenda vizuri!”,alisema Neymar.
Alipoulizwa kuhusu kuondoka kwake Barcelona kwenda PSG, Neymar alisema: “Sikuondoka Barça ili nikawe mchezaji bora duniani nikiwa PSG”.
 
“Messi aliniambia: ‘Kwa nini unaondoka? Unataka kuwa mchezaji bora duniani? Ninaweza kukufanya kuwa mchezaji bora duniani.’
 
“Nilimwambia hapana. Sio hivyo. Kulikuwa na sababu za kibinafsi. Bila shaka PSG kifedha ilikuwa bora zaidi kuliko nilivyokuwa Barcelona na pia kulikuwa na Wabrazili wengi huko.Nilitaka kucheza na Wabrazili wenzangu. Kulikuwa na Thiago Silva, Dani Alves alikuwa amesajiliwa, Marquinhos, Lucas Moura. Wote walikuwa marafiki zangu.” alimaliza Neymar.
#spotileo #spotileoupdates #neymar #messi #romario #barcelona

Related Articles

Back to top button