“Merino ana haki ya kuwa mshambuliaji” – Arteta

LONDON: KOCHA wa Arsenal, Mikel Arteta, amesema kiungo wake Mikel Merino amejitengenezea haki ya kuangaliwa kama mshambuliaji hata pale wachezaji wote wa safu ya mbele watakapokuwa fiti.
Merino, raia wa Hispania aliyesajiliwa kutoka Real Sociedad Agosti 2024, hakuwahi kutumika kama namba 9 kabla ya kuwasili London, lakini alifunga mabao tisa katika msimu wake wa kwanza Emirates akiziba nafasi ya majeruhi Kai Havertz na Gabriel Jesus.
Msimu huu tayari ana mabao 11 kwa klabu na timu yake ya taifa, akichangia kuipandisha Arsenal hadi kileleni mwa Premier League.
Akijibu swali la waandishi kuhusu kama Merino ataendelea kutazamwa kama mshambuliaji hata wote wakiwa fiti, Arteta amesema:
“Amepata angalau fikra hiyo kutokana na kiwango na mchango anaoutoa kwa timu, kwa hiyo jibu ni ‘ndio’.”

Amesema pia wanaweza kumtumia Merino kwenye mstari wa ushambuliaji sambamba na Havertz, Viktor Gyökeres au Jesus, kutokana na mipango iliyowekwa wakati wa majira ya kiangazi.
Arsenal pia inafuatilia hali za kiafya za Declan Rice, Leandro Trossard na William Saliba kuelekea mechi ya Jumamosi dhidi ya Aston Villa walio nafasi ya tatu. Rice alitoka dakika za mwisho kwenye ushindi wa 2-0 dhidi ya Brentford, huku Trossard na Saliba wakikosa mechi mbili zilizopita.
Arteta amesema mazoezi ya Ijumaa jioni yatatoa picha halisi ya upatikanaji wa wachezaji hao, na akasisitiza kuwa msimu huu amejiimarisha kutokana na majeraha yasiyoepukika ya msimu uliopita na maeneo ambayo wanaweza kuyaboresha.




