Matengenezo Uwanja wa Benjamin Mkapa wafikia pazuri

DAR ES SALAAM:KAIMU Mkurugenzi wa Maendeleo ya Michezo, Boniface Tamba amesema matengenezo yanayoendelea katika Uwanja wa Benjamin Mkapa yamefikia pazuri kwa sasa ni zaidi ya robo tatu kuelekea kukamilika.
Amesema hayo Dar es Salaam Leo mbele ya Maofisa Utamaduni na Michezo kutoka mikoa mbalimbali ya Tanzania waliotembelea kujionea miundombinu ya Uwanja huo.
Amesema matengenezo hayo sio tu kwa Uwanja huo bali ule wa Uhuru ambao lengo ni kufikia kiwango bora kinachohitajika na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF).
”Ukarabati wa maeneo yaliyofanyika ni kumewekwa viti vya kisasa 62,000 pamoja na taa za kisasa katika maeneo yanayozunguka uwanja huo, kutengeneza jukwaa Kuu na vyumba vya kubadilishia nguo kwa wachezaji,”amesema.
Amesema mipango mingine wanajenga maeneo ya kupumzikia na Viwanja vya ndani kwa ajili ya michezo kama netiboki, Kikapu, Wavu sambamba na bwawa la Kuogelea.
Tamba aliishukuru Serikali ya awamu ya sita chini ya uongozi wa Rais Dk Samia Suluhu Hassan kwa kuipa kipaumbele sekta ya michezo akisema wamewapendelea wanamichezo.
”Ni wakati wetu sisi wanamichezo kurejesha fadhila kwa serikali kuweka mikakati na kulinda rasilimali zilizowekwa na kufanya vizuri zaidi katika sekta hii ya michezo”,amesema.