Marais watatu wa muziki wa Dansi kutumbuiza jukwaa moja

DAR ES SALAAM: MASHABIKI wa muziki wa dansi nchini wanatarajiwa kushuhudia shoo kubwa ya kihistoria itakayofanyika jijini Dar es Salaam, ikiwakutanisha marais watatu wa muziki wa dansi Tanzania katika jukwaa moja.
Shoo hiyo iliyopewa jina la “3 Kubwa” itawakutanisha wasanii wakubwa wa muziki wa dansi ambao ni Chalz Baba, Christian Bella na Nyoshi El Saadat, wakitumbuiza sambamba na bendi zao.
Katika shoo hiyo, Chalz Baba atatumbuiza akiwa na Twanga Pepeta, Christian Bella atakuwa na Malaika Band, huku Nyoshi El Saadat akiungana na Bogoss Musica.
Tamasha hilo limeandaliwa na Lengos V.I.P kwa kushirikiana na Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (CHAMUDATA), ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuenzi, kukuza na kuendeleza muziki wa dansi nchini, sambamba na kuwakutanisha wasanii wakongwe na chipukizi katika jukwaa moja.
Aidha, shoo hiyo itapambwa na uwepo wa mwanamuziki Elyston Angay, ambaye amewasili nchini kwa ajili ya kushiriki katika burudani hiyo itakayofanyika katika Ukumbi wa Las Carinyo, uliopo Kinondoni, jijini Dar es Salaam.
Usiku huo unatarajiwa kuwa wa kipekee huku ukipambwa na burudani kutoka kwa waimbaji wa sasa na wa zamani wa muziki wa dansi, jambo linaloifanya shoo hiyo kuwa ya kipekee na yenye mvuto mkubwa kwa mashabiki wa muziki huo.




