Featured

Maombolezo ya Pele siku 3, kuzikwa Jan 2

RAIS Jair Bolsonaro wa Brazil anayemaliza muda wake ametangaza siku tatu za maombolezo kufuatia kifo cha nguli wa soka Edson Arantes Do Nascimento ‘Pele’ aliyefariki dunia Disemba 29 huku tarehe ya maziko yake ikithibitishwa.

Pele ambaye atazikwa Januari 2, 2023 alikuwa na umri wa miak 82 na alikuwa akisumbuliwa na saratani ya matumbo.

Bolsonaro, ambaye ataondoka kama rais mnamo Januari 1, 2023 ameandika amri inayosema, kulingana na kitengo cha habari cha Brazil G1: “Maombolezo rasmi yanatangazwa kote nchini, kwa muda wa siku tatu, kuanzia tarehe ya kuchapishwa kwa amri hii, kama ishara ya masikitiko kwa kifo cha Edson Arantes do Nascimento, Pele, mchezaji wa zamani wa soka.”

Taarifa ya klabu ya zamani ya Pele, Santos imesema mwili wa mwanasoka huyo nguli wa wakati wote utaagwa kwenye uwanja Urbano Caldeira uliopo eneo la Belmiro katika jiji la Sao Paulo ambako aliichangamsha dunia.

“Mwili wa Pele utatoka moja kwa moja Hospitali ya Albert Einstein kwenda uwanjani Januari 2 na jeneza litawekwa katikati ya nyasi,’ imesema taarifa ya Santos.

Edson Arantes Do Nascimento ‘Pele’ wa Brazil akishangalia ubingwa wa Kombe la Dunia baada ya Brazil kuifunga Italia mabao 4-1 kwenye uwanja wa Azteca, Mexico City, Mexico mwaka 1970..

Pele alikuwa mmoja wa wanasoka maarufu wa wakati wote akishinda kombe la dunia mara tatu, 1958, 1962 na 1970.

Pia anabaki mfungaji wa mabao mengi zaidi wa wakati wote timu ya taifa ya Brazil sambamba na Neymar Jr wa mabao 77 na alifunga mabao 643 katika michezo 659 katika klabu ya Santos.

Wakati huo huo Rais Samia Suluhu Hassan ametuma salamu za rambirambi kutokana na kifo cha Pele.

Kupitia ukurasa wake rasmi wa Twitter Rais Samia amesema:”Nimepokea kwa masikitiko taarifa za kifo cha Mwanasoka wa Karne kutoka Brazil Edson Arantes do Nascimento “Pelé”. Mchango wake katika soka Duniani utakumbukwa daima. Pole kwa Rais wa Brazil @jairbolsonaro, familia & mashabiki wote wa soka. Mungu amweke mahali pema peponi, Amina.”

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button