Madrid yampata ‘Yamal’ wao

MADRID: Real Madrid imetangaza kuwa imefikia makubaliano ya kumsajili kiungo kinda wa River Plate Franco Mastantuono kwa mkataba ambao utamfanya kinda huyo kuvinjari viunga vya Santiago Bernabeu kwa misimu sita ijayo,
Katika taarifa yake juu ya usajili huo Madrid imesema Mastantuono mwenye umri wa miaka 17 atajiunga mapema mwezi Agosti kwenye msimu mpya wa LaLiga, hii inamaanisha kuwa atachezea River kwenye Kombe la Dunia la Klabu. Michuano ambayo Madrid pia wanacheza.
Mastantuono ni mchezaji wa tatu kusajiliwa na Madrid baada ya kuwaongeza mabeki Trent Alexander-Arnold na Dean Huijsen. Mastantuono aliichezea timu ya taifa ya Argentina kwa mara ya kwanza wiki iliyopita, akitokea benchi katika ushindi wa 1-0 dhidi ya Chile katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Dunia 2026.
Madrid inajaribu kurejesha makali yake chini ya kocha mpya Xabi Alonso baada ya kupoteza mataji yao ya LaLiga na Ligi ya Mabingwa msimu uliopita. Mabadiliko hayo yanahusisha pia kuanza maisha bila kiungo wao mkabaji Luka Modric, ambaye ataondoka Madrid baada ya Kombe la Dunia la Klabu.