Kwingineko

Leverkusen yaiondoa Dortmund DFB Pokal

DORTMUND: MABINGWA wa zamani wa Bundesliga Bayer Leverkusen wamewatupa nje wababe Borussia Dortmund katika hatua ya 16-bora ya Kombe la Ujerumani baada ya ushindi wa 1-0 ugenini, Jumanne, kwa bao pekee la Ibrahim Maza.

Maza alifunga dakika ya 34, akiwaweka mabingwa hao wa Kombe la Ujerumani wa 2024 kwenye njia ya ushindi na kulipa kisasi dhidi ya Dortmund, waliowafunga mabao 2-1 kwenye Bundesliga siku tatu zilizopita.

Ushindi huo unawapeleka Leverkusen robo fainali ya kombe hilo, ambako wataungana na RB Leipzig, waliowachapa Magdeburg 3-1, pamoja na Hertha Berlin na St Pauli, waliotangulia kufuzu mapema Jumanne.

Wababe Dortmund na Leverkusen wamekutana mara 109 kwenye mashindano yote tangu miaka ya 1950, hii ikiwa mara yao ya kwanza kukutana kwenye Kombe la Ujerumani.

Dortmund walipata kilio cha mapema baada ya ombi lao la penalti kukataliwa, wakati beki wa zamani wa Liverpool, Jarell Quansah, alipoonekana kumwangusha Carney Chukwuemeka ndani ya eneo la hatari.

Maza, ambaye pia alifunga katika ushindi wa kushangaza wa 2-0 dhidi ya Manchester City kwenye Ligi ya Mabingwa Ulaya, aliipita safu ya ulinzi ya Dortmund kwa ustadi mkubwa kabla ya kupiga shuti kali lililowapa Leverkusen uongozi.

Dortmund walipata nafasi ya kusawazisha dakika za mwisho za muda wa nyongeza, lakini kichwa cha Karim Adeyemi kilipita sentimita chache tu pembeni ya mwamba.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button