Kriketi yajipanga kufuzu Kombe la Dunia

DAR ES SALAAM: Timu ya Taifa ya Kriketi imeanza maandalizi ya kujiweka imara kwa ajili ya shindano la mwisho la kufuzu Kombe la Dunia litakalofanyika Nigeria Machi 26, mwaka huu.
Tanzania itakutana na wababe wa michuano hiyo Namibia, Uganda, Nigeria,Kenya na Siera Leon ambapo anahitajika mshindi mmoja wa kuwakilisha michuano ya Dunia itakayofanyika mwakani Namibia na Zimbabwe.
Akizungumza na SpotiLeo Kocha Mkuu Imran Nackerdien alisema wanaendelea vizuri na maandalizi kuhakikisha sio tu wanakwenda kushiriki bali kupambana na kushinda ili kupata nafasi hiyo moja.
“Hii ni michuano muhimu kwetu, tunajua hatua hii ya mwisho huenda ikawa migumu, jambo kubwa kwetu ni kufanya maandalizi mazuri na ya kutosha ili kwenda kushinda,”alisema.
Nahodha wa timu hiyo Laksh Bakrania alisema kama wachezaji wako tayari kwenda kupigania bendera ya Taifa na kwamba hakuna wanayemuogopa wala kumhofia.
Alisema licha ya kwamba wapinzani hao wote ni bora watapambana kwa jasho au damu kutimiza lengo lao la kushinda mechi zao zote na kukata tiketi ya kwenda kuwakilisha Kombe la Dunia.
Alisema timu hizo walishakutana kwenye hatua za awali hivyo wanajuana vizuri.