Nyumbani

Kocha Yanga ataja kilichomvuta Yanga

DAR ES SALAAM. KOCHA mpya wa Klabu ya Yanga Romain Folz ameweka wazi kuwa uamuzi wake wa kujiunga na mabingwa hao wa Ligi Kuu Tanzania Bara umetokana na mvuto mkubwa wa mashabiki wa timu hiyo, ambao ameahidi kuwapa furaha msimu ujao.

Folz amechukua mikoba iliyoachwa na Miloud Hamdi aliyetimkia Ismaily SC ya Misri baada ya kuipa Yanga mataji.

Akizungumza kwa mara ya kwanza tangu athibitishwe rasmi kuchukua mikoba ya ukufunzi, kocha huyo amesema:

“Nataka mashabiki wajue kuwa moja ya sababu kubwa zilizonivutia kuja hapa ni wao. Sapoti ya mashabiki wa Yanga ni ya kipekee na imekuwa sehemu ya uamuzi wangu,”

Akiwa na malengo makubwa, Kocha huyo amesema msimu ujao utakuwa mrefu, na timu hiyo itashiriki michuano mingi – hivyo ni muhimu kwa mashabiki kuwa bega kwa bega na kikosi chao.

“Tuna mashindano mengi, tuna mechi nyingi za kushinda. Tunahitaji sapoti yao kuanzia sasa hadi mwisho wa msimu. Kila ushindi tutakaopata si wetu pekee, bali ni wao pia tunashinda pamoja,” alisema.

Ameongeza kuwa anatamani kuona mashabiki wake haraka iwezekanavyo na kushiriki nao furaha, changamoto na mafanikio ya msimu ujao.

Yanga imekuwa na msimu wa mafanikio katika miaka ya hivi karibuni, na ujio wa kocha mpya unaibua matumaini mapya kwa mashabiki na wadau wa soka nchini. Mashabiki sasa wanasubiri kwa hamu kuona aina ya mpira na mafanikio atakayowaletea.

 

Related Articles

Back to top button