FeaturedLigi KuuNyumbani

Kocha Kagera Sugar amfagilia Fei toto

KOCHA Mkuu wa Kagera Sugar, Francis Baraza  amemwagia sifa kiungo mshambuliaji wa Yanga, Feisal Salum ‘Fei toto’ akisema ni mchezaji mwenye uwezo wa kucheza ligi yoyote duniani kutokana na kipaji cha kusakata soka alicho nacho.

Mchezaji huyo kwa sasa amekuwa gumzo nchini kutokana na uwezo mkubwa alionao akiwa na timu yake ya Yanga na timu ya taifa, Taifa Stars, ambapo amekuwa akitoa mchango mkubwa ikiwamo kufunga mabao na kutoa pasi za mabao.

Akizungumza na gazeti hili, Baraza alisema amekuwa akimfuatilia kwa karibu mchezaji huyo na amegundua ni mwenye kipaji cha hali ya juu na ana anaweza kufika mbali kutokana na kipaji alichonacho, kitu cha msingi kwake ni kuzidisha bidii na kusikiliza makocha wake.

“Feisal wa Yanga ni mchezaji mwenye kipaji cha juu sana, kama atazingatia maelekezo kutoka kwa makocha wake atafika mbali, kipaji alichonacho anaweza kucheza ligi ya nchi yoyote hapa Afrika na hata Ulaya,” alisema Baraza.

Kocha huyo alisema Tanzania ni taifa lililojaaliwa vipaji vingi vya soka isipokuwa tatizo kubwa la wachezaji wanakosa nidhamu na kufuata makundi jambo linalochangia kuua vipaji vyao.

Alisema mbali ya makundi, kingine kinachochangia vipaji vya wachezaji wa Tanzania kupotea ni kutokuwasikiliza makocha wao na kutozingatia maadili ya mchezo.

Baraza pia amejivunia mafanikio ya kiungo wa kimataifa wa Tanzania anayecheza soka la kulipwa kwenye klabu ya Maccabi Tel Aviv ya  Israeli, Novatus Dismas kuwa siri kubwa ya mafanikio aliyonayo ni usikivu wa  anachoelekezwa na kocha wake akiwepo yeye wakati wakiwa pamoja Biashara United ya  Mara.

Related Articles

Back to top button