“Kipigo hiki kitufunze unyenyekevu” – Glasner

LONDON: Kocha wa Crystal Palace, Oliver Glasner, amesema kipigo cha 1-0 nyumbani dhidi ya AEK Larnaca kutoka Cyprus katika michuano ya Europa Conference League ni funzo kwa timu yake kubaki wanyenyekevu.
Palace walikuwa wanacheza mechi yao ya kwanza ya Ulaya katika historia ya miaka 101 ya klabu hiyo, lakini bao la Riad Balic mapema kipindi cha pili lilizima furaha ya mashabiki uwanjni Selhurst Park.
Wakati Crystal Palace wakishika nafasi ya nane kwenye Ligi Kuu ya England wakiwa kwenye mwenendo mzuri, Larnaca wao wanashika nafasi ya tano kwenye ligi kuu ya Cyprus.

“Tutajifunza kutokana na hili, wachezaji wamepata somo. Ni usiku wa kukatisha tamaa, lakini labda tulihitaji hali kama hii ili tubaki wanyenyekevu. Watu huambiwa kuwa ukiwa unacheza Premier League, unaweza kushinda Conference League kirahisi lakini si ukweli. Inatufundisha kujitazama upya na kubaki wanyenyekevu.”
“Sijawahi kuona timu mpya ikishinda mashindano haya kwa ushiriki wa mara ya kwanza. Sidhani kama ni rahisi hivyo,” amesema Glasner baada ya mchezo huo kumalizika usiku wa kuamkia leo.
Crystal Palace sasa wanatarajia kuvaana na vinara wa ligi Arsenal Jumapili kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya England unaovuta hisia za watu wengi.




