Kwingineko

Kim Kardashian amteua Msenegali kusimamia mradi wake

NEW YORK: MJASIRIAMALI maarufu Kim Kardashian amemteua Diarrha N’Diaye, ambaye ni Mmarekani mwenye asili ya Senegal na mwanzilishi wa chapa ya urembo inayosifika Ami Colé, kuwa Makamu wa Rais wa Urembo na Manukato kwa ajili ya mradi wake mpya wa Skims Beauty unaotarajiwa kuzinduliwa hivi karibuni.

Uteuzi huu, ambao umetangazwa na ‘The Cut’ na ‘Cosmopolitan’, unachukuliwa kama hatua kubwa kuelekea ujumuishaji (inclusivity) katika tasnia ya urembo duniani.

Katika tamko lake, N’Diaye alisema:
“Nimezunguka sana katika tasnia hii, na ninafuraha kuleta uzoefu wangu wote katika timu ya Kim. Mbingu ndiyo mpaka wetu, na nataka kila msichana mdogo mwenye ngozi ya kahawia ajue kwamba inawezekana.”

N’Diaye amejijengea sifa kwa kujitolea kwake kutengeneza bidhaa rahisi na rafiki kwa ngozi yenye rangi ya melanin, zinazoadhimisha uzuri wa asili na urithi wa Kiafrika. Kupitia Ami Colé, amekuwa sauti muhimu katika kuhimiza uwakilishi halisi na uelewa wa urembo unaoheshimu utofauti.

Kwa upande wa Kardashian, ambaye chapa yake ya Skims tayari imeleta mapinduzi katika mavazi ya kubana (shapewear) amesema kumleta N’Diaye ni ishara ya hatua mpya kuelekea uhalisia na mitazamo mbalimbali ya kidunia.

Zaidi ya biashara, uteuzi huu unaonekana kama ushindi wa kimaana kwa wanawake wa Kiafrika katika sekta za ubunifu za kimataifa.

Kadiri mashabiki wakisubiri uzinduzi wa Skims Beauty, macho yote sasa yameelekezwa kwa Diarrha N’Diaye kuangalia ni nini atakachounda chini ya chapa yenye ushawishi mkubwa ya Kardashian, na jinsi atakavyoinua mjadala wa uwakilishi katika ulimwengu wa urembo.

Related Articles

Back to top button