Katy Perry ashindwa kisheria na Katie Perry

AUSTRALIA : Mahakama Kuu ya Australia imetoa ushindi kwa mbunifu wa mavazi wa nchini humo Katie Perry, katika mgogoro wa muda mrefu wa nembo ya biashara dhidi ya nyota wa muziki wa pop kutoka nchini Marekani Katy Perry.
Mbunifu huyo alikuwa amemshtaki mwanamuziki huyo maarufu duniani akidai kuwa alikiuka haki ya matumizi ya jina ‘Katie Perry’, ambalo tayari alikuwa amelisajili kwa biashara ya mavazi kabla mwimbaji huyo hajapata umaarufu mkubwa duniani.
Hata hivyo, Katy Perry alidai kuwa kufikia mwaka 2008 muziki wake ulikuwa tayari umesambaa kwa kasi duniani, kipindi ambacho mbunifu huyo ndipo alianza kuuza mavazi yake, na hivyo aliomba nembo ya biashara hiyo ifutwe.
Awali mahakama moja nchini Australia mwaka 2024 ilimpa ushindi mwanamuziki huyo, lakini katika rufaa iliyofuata Mahakama Kuu imeamua kuwa hakuna uwezekano wa watumiaji kuchanganya chapa ya mavazi ya mbunifu huyo na mwanamuziki maarufu duniani.
Uamuzi huo sasa unamruhusu mbunifu huyo kuendelea kuuza mavazi yake chini ya jina la ‘Katie Perry’.




