KAMUNGO: Mtanzania anayetamba soka Marekani

USIKU wa kuamkia Agosti 8, mwaka huu ulikuwa wa kihistoria mno kwa mshambuliaji wa timu ya FC Dallas ya Marekani, Bernard Kamungo anayeelezwa kukulia kwenye kambi
ya wakimbizi ya Nyarugusu, Kasulu, Kigoma.
Kamungo mwenye miaka 21, alijitambulisha kwenye uso wa dunia na Afrika baada ya kufunga bao zuri kwenye mechi yao dhidi ya Inter Miami katika michuano mipya ya Kombe la Ligi inayojumuisha timu za Ligi Kuu ya Marekani (MLS) na Ligi Kuu ya Mexico.
Haikuwa rahisi kwani katika mechi dhidi ya timu iliyojaa nyota wengi waliozoa kila kitu katika soka la dunia; Sergio Busquets, Jordi Alba na mshindi wa Ballon d’Or mara saba, Lionel Messi, Kamungo akaonesha ubora wake na kuwa gumzo.
Ni katika mechi hiyo ambayo bei za tiketi zilipanda kwa viwango ambavyo havijawahi kuonekana katika historia ya klabu hiyo kutokana na uwekezaji wa wachezaji uliofanywa na mmiliki wa Miami, David Beckham kuelekea msimu ujao.
Kwenye mechi hiyo ya hatua ya 16 bora, nahodha wa Miami, Messi alifunga bao dakika ya sita kabla ya Facundo Quignon kuchomoa dakika ya 37 na kisha Kamungo naye kufanya yake dakika ya 45.
Cha kuvutia zaidi, Kamungo alifunga bao hilo na kuiweka mbele Dallas kwa mabao 2-1 mpaka mapumziko. Jesus Ferreira alimpenyezea Kamungo pasi safi kwenye eneo la hatari.
Kwa utulivu, winga huyo aliwachambua mabeki wawili kabla ya kumtoka kipa na kuujaza mpira wavuni huku mtangazaji akisema: “Ndoto inaendelea kwa Kamungo.” Hata hivyo, mechi hiyo haikuwa upande wa Dallas kwani dakika 90 zilikamilika kwa sare ya mabao 4-4 kabla ya Miami kushinda kwa matuta 5-3 na kusonga mbele.
ZAMU YA KAMUNGO
Kwa bao hilo ni wazi Kamungo anakuwa miongoni mwa wachezaji wa Tanzania waliofunga kwenye mechi iliyojaa nyota wakubwa duniani kama alivyofanya nahodha wa Taifa Stars, Mbwana Samatta alipofunga mbele ya Anderlecht iliyokuwa na beki, Vincent Kompany.
Au alivyoifunga Manchester City kwenye Uwanja wa Wembley, England au lile bao lake dhidi ya Liverpool kwenye michuano ya Uefa.
Baada ya bao hilo, Kamungo alisema: “Sijui hata nielezee vipi sababu sijawahi kufunga mbele ya Imani (kaka yake aliyekuwa uwanjani, Uwanja wa Toyota), ilikuwa mara ya kwanza kufunga mbele yake, na ilikuwa dhidi ya Messi. “Nilimgeukia na nikamwambia tu, ‘bao hili lilikuwa kwa ajili yako.’ Kwa sababu alinifanyia mengi kufika hapa nilipo sasa hivi. Nina furaha sana ameniona nikifunga.”
ALIFIKAJE MAREKANI
Kamungo akiwa na kaka yake na familia yao huko Kigoma waliendelea na maisha mengine lakini hayakuwa ya kuridhisha, kupitia mahojiano aliyoyafanya na mwandishi Garrett Melcer, Kamungo anasema ilikuwa ngumu kuupata mpira wa kuchezea, hivyo waliunda mpira wa makaratasi kukata kiu yao.
Anafafanua kwamba alicheza mpira kama jambo la kujifurahisha tu, lakini hakuwa na ndoto ya kwamba siku moja atakuwa mchezaji wa kulipwa. Mwaka 2017 akiwa na miaka 14 kwa msaada wa Kamati ya Kimataifa ya Uokoaji, yeye na familia yake walihamia Abilene, Texas, Marekani.
“Ilikuwa ajabu kwangu kwa sababu tulipofika Abilene, familia yangu ilipata kitu cha kutulisha. Na hiyo ndiyo yote niliyokuwa nikitafuta. Tanzania ilikuwa vigumu kupata kitu cha kukulisha. Lakini tulipofika Abilene, nilianza kula kama kawaida, sasa ningeweza kula
mara tatu au nne kwa siku, chochote nilichotaka.”
KAKA YAKE ALIVYOMPIGANIA
Kamungo anamtaja kaka yake Imani kama chachu ya mafanikio yake kwani alikuwa akiona kipaji ndani yake na kumsukuma kucheza soka alipoanza katika shule ya Abilene High School.
Baada ya kumaliza shule, Imani alianza harakati za kutafuta timu ili Kamungo
akafanye majaribio ambapo walipata timu mbili moja ikihitaji malipo ya Dola za
Marekani 90 na nyingine Dola 500.
Hata hivyo, Kamungo alimshauri Imani walipe ya Dola za Marekani 90 maana ni ndogo na hawatajuta hata ikitokea wamefeli kwa kuwa ni kiasi kidogo, walikubaliana kufanya hivyo.
Wakaenda kujaribu bahati kwenye timu ya akiba ya Daraja la Tatu ya North Texas, ambapo kiwango chake kilimvutia kocha Eric Quill na kumchagua yeye na wengine watatu kupewa mkataba na timu hiyo.
Nyota yake ilianza kung’ara katika mechi yake ya kwanza tu dhidi ya Fort Lauderdale alipoingia dakika ya 71 kuchukua nafasi ya Hope Avayevu ambapo dakika nane baadaye akafunga bao lake la kwanza katika mechi iliyoisha kwa ushindi wa mabao 4-2.
Kamungo aliendeleza moto na kuwa nyota wa kikosi kabla ya Agosti, 2022 kupewa kandarasi ya miaka minne na FC Dallas na Aprili 15, mwaka huu akafunga bao lake la kwanza dhidi ya Real Salt Lake kwenye dakika ya 88 katika ushindi wa mabao 2-1.
TANZANIA ILISHAMWONA
Kabla ya kuwa gumzo, Taifa Stars chini ya kocha Adel Amrouche ilimwita Kamungo kwa mara ya kwanza kwenye kikosi hicho Juni, mwaka huu kilichokuwa kikijiandaa kuvaana na Niger kuwania kushiriki michuano ya Mataifa Afrika (Afcon).
Kamungo anasema: “Timu ya taifa niliitwa mara ya mwisho (dhidi ya Niger) lakini moja ya sababu ya kutoonekana na wengi wanajiuliza ilikuwaje, ni masuala ya pasi ya kusafiria, pasi ilichelewa kidogo ndio maana ikashindikana ila naamini kama mambo yatakwenda sawa, mwezi ujao mechi ya Algeria nitakuwepo, ikitegemea taifa litakavyoamua lakini niko tayari kuitumikia Tanzania.”
Mchezaji huyo anayevaa jezi namba 77 kwa sasa kutoka namba saba aliyokuwa akiivaa North Texas, amefunga mabao 23 katika mechi 54 za mashindano ya klabu mpaka sasa, akitajwa na vyombo vya Marekani kuwa ni kijana mwenye kipaji kikubwa kinachoendelea
kuimarika kila kukicha.