Muziki

Jonathan Budju kuachia EP mpya ‘Ebenezer’

MWIMBAJI nyota wa muziki wa Injili anayeishi nchini Canada, Jonathan Budju, anatarajia kuachia rasmi albamu yake fupi (EP) iitwayo Ebenezer mnamo Julai 25, 2025.

Akizungumza na Spoti Leo, Budju alisema kuwa tayari amefanya hafla maalum ya kusikiliza (listening party) ya EP hiyo nyumbani kwake nchini Canada, ambapo watu wachache waliopata nafasi ya kuisikiliza wameipokea kwa shangwe na furaha.

“Mapokezi yamekuwa mazuri sana. EP hii ina nyimbo zenye mguso wa kipekee ambazo naamini zitabadilisha maisha ya watu wengi. Nina imani kuwa mashabiki wataweza kubarikiwa kupitia ujumbe uliomo,” amesema Budju ambaye pia anajulikana kwa jina la Son of God.

Ebenezer inajumuisha nyimbo zilizorekodiwa kwa lugha ya Kiswahili, Kiingereza na Kifaransa, jambo linalomuwezesha kuwafikia wasikilizaji kutoka sehemu mbalimbali duniani. Budju ni miongoni mwa waimbaji wa Injili waliopata umaarufu mkubwa ughaibuni kwa kutumia muziki kama njia ya kufikisha ujumbe wa imani na matumaini.

EP hiyo itapatikana kwenye majukwaa yote ya kidijitali yanayouza na kuruhusu upakuaji wa muziki duniani, na Budju amewataka mashabiki wake kujiandaa kupokea kile alichokiita “zawadi kutoka kwa Mungu.”

Related Articles

Back to top button