CHAN

Hamasa ya CHAN 2024 yazidi kupambana moto, 

mashabiki waitwa kwa Mkapa

DAR ES SALAAM: WAKATI Tanzania ikijiandaa kwa mashindano ya CHAN 2024, hali ya hamasa imepamba moto kote nchini huku viongozi wa michezo wakitoa wito kwa Watanzania kujitokeza kwa wingi kushangilia Taifa Stars.

Mashindano hayo ya wachezaji wanaocheza ligi za ndani yataanza rasmi Agosti 2, mwaka huu kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, ambapo Tanzania itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya Burkina Faso.

Ofisa Habari wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Clifford Ndimbo, amesema kuwa michuano hiyo ni fursa adhimu kwa Taifa Stars kuandika historia mbele ya mashabiki wake.

“Tumepewa bahati ya kipekee ya kuwa wenyeji wa mechi ya ufunguzi. Kwa viingilio vya kati ya shilingi 2,000 hadi 10,000, kila Mtanzania ana nafasi ya kushuhudia historia. Huu ni wakati wa kuonesha uzalendo,” alisema Ndimbo katika tukio la hamasa lililofanyika Stendi ya Magufuli Mbezi.

Ndimbo pia alitoa wito wa kuvaa jezi za Taifa Stars kama ishara ya mshikamano wa kitaifa, akisisitiza kuwa mashindano haya ni ya Watanzania wote bila kujali mapenzi ya klabu.

Kwa upande wake, Msemaji wa Simba SC, Ahmed Ally, alisema kuwa CHAN 2024 si mashindano ya TFF pekee bali ni tukio la kitaifa linalohitaji ushiriki wa kila Mtanzania.

“CHAN si ya TFF wala klabu yoyote – ni ya Watanzania wote. Leo si Simba wala Yanga, leo ni Taifa Stars. Tuache utani, tushikamane kwa ajili ya timu yetu ya taifa,” alisema Ahmed.

Ahmed alisisitiza kuwa Simba SC iko tayari kutoa sapoti kwa namna yoyote ili Taifa Stars ifanikishe ndoto ya kutwaa taji hilo mbele ya mashabiki wa nyumbani.

Christina Mwagala, Msemaji wa Tabora United na mmoja wa wahamasishaji wa Taifa Stars, alieleza kuwa huu ni wakati wa kuungana na kuonesha upendo wa kweli kwa nchi.

“Tunapaswa kuwa wamoja – iwe unaishi Mbeya, Mwanza au Tabora, huu ni wakati wetu wa kuja pamoja kama taifa. Tuvae jezi, twende uwanjani, tuimbe na tuwashangilie vijana wetu,” alisema Mwagala.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button