Eric Omondi apata Jeraha la yonga siku ya kwanza ya matembezI ya hisani

NAIROBI:MCHEKESHAJI maarufu wa Kenya, Eric Omondi, amepata jeraha la nyonga katika siku ya kwanza ya matembezi yake ya hisani kutoka Nairobi hadi Mombasa.
Eric, anayefanya safari hiyo ya kilomita 486 kwa lengo la kuchangisha fedha za kujenga Kituo kipya cha ‘Help and Rescue’, alifanikiwa kutembea kilomita 68 katika siku ya kwanza na kuhitimisha safari yake ya siku hiyo mjini Machakos.
Hata hivyo, matembezi hayo yenye changamoto kubwa kimwili yalimwacha akiwa amechanika mishipa (ligaments) katika mguu wake wa kushoto pamoja na nyonga.
Licha ya jeraha hilo, Eric amesema ataendelea na safari hiyo hadi afike Mombasa, akitarajia kuikamilisha ifikapo Siku ya Wapendanao (Valentine’s Day).
“Lazima tutafika Mombasa hata kama ni by fire. Leo nimechanika mishipa kwenye mguu wangu wa kushoto na nyonga, lakini kesho tutaendelea hata kama tutakuwa tunatambaa. Unaweza kutembea nami kwa kutuma chochote unachoweza,” aliandika kupitia ukurasa wake wa Instagram.
Aidha, aliwahimiza wanaomuunga mkono kuchangia kwa kununua kilomita za safari hiyo, ambapo kilomita moja inagharimu Sh15,000.
“Kama unaona ninachoka sana, unaweza kuninunulia kilomita; kilomita moja ni Sh15,000. Ukifanya hivyo, sitalazimika kutembea umbali huo,” aliongeza.
Mpango huo unalenga kuanzisha kituo cha kwanza cha kimwili cha ‘Help and Rescue’ chini ya taasisi yake ya “Sisi kwa Sisi”.
Kwa mujibu wa Eric, kituo hicho kitakuwa na zahanati, shule ya sekondari ya bure, ghala la kuhifadhi misaada pamoja na magari mawili ya wagonjwa (ambulance) ili kuwasaidia Wakenya wanaohitaji msaada.
Safari hiyo ilianza katika Uwanja wa Nyayo jijini Nairobi, ambapo ilizinduliwa rasmi na mwimbaji wa nyimbo za injili Daddy Owen huku akisindikizwa na umati mkubwa wa mashabiki.




