Curaçao Kwenda WC na Historia

KINGSTON: TIMU ya Taifa ya Curaçao imefanikiwa kuwa timu ya taifa dogo zaidi kwa idadi ya watu kuwahi kufuzu Kombe la Dunia baada ya kupata sare ya 0-0 dhidi ya Jamaica jana Jumanne na itaungana na mataifa mengine ya CONCACAF ya Panama na Haiti ambayo pia yamefuzu
Curaçao ilimaliza michuano yakufuzu ikiwa timu pekee ambayo haikupoteza mchezo katika mashindano kuongoza Kundi B kwa pointi 12, na hivyo kufuzu Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza katika historia yake.
Curaçao ilipata matokeo hayo ya kihistoria licha ya kutokuwa na kocha wao Dick Advocaat kwenye benchi. Kocha huyo mwenye umri wa miaka 78 alikosa mchezo huo muhimu kwa sababu alilazimika kurejea Uholanzi mwishoni mwa wiki kutokana na sababu za kifamilia.
Advocaat aliwahi kuinoa timu ya taifa ya Uholanzi kwa vipindi vitatu tofauti na aliwahi pia kuifundisha Korea Kusini, Ubelgiji na Urusi kabla ya kuchukua kazi ya kuinoa Curaçao.




