Chino Kidd kusambaza upendo kwa wasanii wa singeli

DAR ES SALAAM:MSANII maarufu wa Bongo Fleva, Isaya Michael Mtambo almaarufu Chino Wanna Man, ameweka wazi dhamira yake ya dhati ya kuwasaidia wasanii wa muziki wa singeli nchini.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram, Chino ambaye kwa sasa anatikisa anga ya muziki na vibao moto kama Tiririka, Koko na Kibabe, ameposti picha akiwa na mama yake mzazi huku akiambatanisha ujumbe maalumu unaowataka mashabiki wake kuwataja wasanii wa singeli wanaowakubali.
Katika ujumbe huo, Chino amewaomba mashabiki wake kuwataja wasanii wa singeli kutoka mitaani mwao na kuwaelekeza watume kazi zao kwenye namba ya WhatsApp aliyoweka wazi. Ujumbe huo unasomeka:
“Kwa heshima na urahisi, kila ambae unaona post hii mtag msanii wako wa singeli unayemkubali mtaani kwako na aweze kutuma hiyo nyimbo yake kwenye hii number 062716458505. Zingatia quality ya audio yako na ufundi wa idea yako iwe kalii. Asante.”
Chino ameeleza kuwa hatua hiyo ni sehemu ya harakati zake za kusaidia kukuza vipaji vya vijana kupitia muziki, hasa kwenye miondoko ya singeli ambayo inaendelea kushika kasi nchini Tanzania. Ameongeza kuwa yeye ni kijana anayeamini katika mafanikio ya pamoja na kuipa heshima nchi yake kupitia sanaa.
Hatua hii ya Chino inaonesha wazi moyo wake wa uzalendo na nia ya dhati ya kuendeleza muziki wa Kitanzania kwa kuunga mkono wasanii chipukizi. Bila shaka, huu ni mwaliko wa dhati kwa wasanii wa singeli wenye vipaji kuwasilisha kazi zao na kuchangamkia fursa hiyo adimu.
Je, una msanii wa singeli unayemkubali mtaani kwako? Mtag sasa na mpe nafasi ya kung’ara kupitia jukwaa la Chino Wanna Man!