Billnass awaonya vijana wenye vipaji

MSANII maarufu wa Bongo Fleva, William Lyimo ‘Billnass’, amewapa ushauri vijana wadogo wenye vipaji wanaotamani kuingia kwenye tasnia ya muziki na sanaa kwa ujumla, akiwahimiza kumtanguliza Mungu mbele ya safari yao.
Kupitia Insta Story yake, Billnass amesisitiza kuwa mafanikio katika kazi hizi yanahitaji uvumilivu mkubwa kwa sababu tasnia hiyo imejaa changamoto nyingi.
“(To all young people), wadogo zangu na rafiki zangu mliojaliwa vipaji mbalimbali kabla ya kuingia kwenye tasnia inayohusiana na umaarufu Tanzania, muombe sana Mungu akupe uvumilivu na roho ya kustahamili,” aliandika Billnass.
Akiendelea kufunguka, Billnass ameleza kuwa changamoto hizo zinajumuisha vita, usaliti, ushetani na dhuluma kutoka kwa baadhi ya wadau wa sanaa wakiwemo mameneja, kampuni za usambazaji (distribution companies) na hata labels.
Kwa mujibu wa msanii huyo, ingawa wengi huingia kwenye sanaa kwa matarajio ya utajiri na mafanikio, ukweli ni kwamba kuna hatari zaidi za kupatwa na msongo wa mawazo, magonjwa ya akili, kuchanganyikiwa na hata kupoteza maisha.
Hivyo amewataka kujiandaa kukabiliana na maisha watakayokutana nayo katika Sanaa na watakapokuwa maarufu.



